Rais wa Marekani Joe Biden na Mwanasheria Mkuu wa Serikali Merrick Garland wamepanga kuzungumza Alhamisi juu ya hatua mpya zinazo kusudiwa kushughulikia ghasia za bunduki nchini Marekani.
Kabla ya matamshi yao, White House ilitoa maelezo ya baadhi ya mipango hiyo, ikitaja ghasia za bunduki kuwa janga la afya ya umma.
Kitendo kimojawapo ni sheria inayopendekezwa kutoka wizara ya Sheria kuzuia kuenea kwa kile kinachoitwa bunduki zisizoonekana ambazo hazina namba na ni ngumu kwa Polisi kufuatilia wakati zinatumiwa katika uhalifu.
Idara ya Sheria pia inapanga kutoa mfano wa kile kinachojulikana kama kiashiria cha hatari ambacho huwapa wanafamilia na watekelezaji wa sheria uwezo wa kuomba mahakama kumzuia kwa muda mtu anayeonekana kuwa hatari kwake au kwa mtu mwingine kuweza kumiliki bunduki.
Mfano huo umekusudiwa kuyapa majimbo moja moja kianzio cha kutunga sheria zao wenyewe.