Viongozi wa Marekani wamelaani mauaji yaliotokea katika mji wa Boulder Colorado nchini humo siku ya Jumatatu.
Ufyatuaji wa risasi wa kwenye duka moja katika mji huo umeuwa watu 10 akiwemo afisa wa polisi ailyekuwa wa kwanza kufika kwenye eneo la tukio wakati mshukiwa wa shambulizi hilo alijeruhiwa na kukamtwa muda mfupi baadaye.
Polisi mjini humo hawajatoa ripoti za kina kuhusiana na shambulizi hilo lililotokea saa tisa za jioni kwenye duka la King Soopers kwenye kitongoji cha Table Mesa mjini Boulder ulioko takriban kilomita 45 kaskazini magharibi mwa mji mkuu wa jimbo hilo wa Denver.
Tukio la Jumatatu ni la pili kutokea hapa Marekani ndani ya kipindi cha wiki moja baada ya lile la Jumanne wiki iliyopita ambapo watu wanane waliuwawa mjini Atlanta wakiwemo wanawake 6 wenye asili ya Asia.
Mwanaume mwenye umri wa miaka 21 tayari amefunguliwa mashitaka kutokana na shambulizi hilo. Mkuu wa polisi wa Boulder Maris Herold amesema kuwa miongoni mwa watu waliokufa ni afisa wa polisi Eric Talley mwenye umri wa miaka 51.
Mkuu wa habari wa Ikulu ya Marekani Jen Psaki kupitia ujumbe wa twitter amesema kuwa Rais Joe Biden amefahamishwa kuhusu tukio hilo na kwamba ataendelea kuarifiwa kadri uchunguzi unavyoendelea.
Taarifa zimeongeza kusema kuwa mshukiwa aliyekamatwa ndiye pekee aliyenusurika wakati wa shambulizi hiyo japo amejeruhiwa vibaya .