Mapigano makali yanaendelea Jumamosi kaskazini magharibi mwa Kyiv, mji mkuu wa Ukraine, na katika miji mingine kadhaa huku majeshi ya Russia yakijikusanya kilomita 25 kutoka mji mkuu.
Vingora vya tahadhari kwa mashambulizi ya anga vilisikika katika miji kadhaa usiku, vikiwaonya wakazi juu ya kuwepo njiani mashambulizi ya anga.
Wizara ya Ulinzi ya Russia inasema imekiharibu kituo cha kijeshi cha anga cha Ukraine karibu na mji wa Vasylkiv. Ghala ya silaha karibu na hapo pia imeelezwa kuwa iliharibiwa.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Ukraine inasema majeshi ya Russia Jumamosi waliushambulia msikiti mjini Mariupol ambako watu 80 walikuwa wamejihifadhi. Kati ya waliokuwa msikitini walikuwa wanatokea Uturuki.
Njia kadhaa za misaada ya kibinadamu zilitarajiwa kufunguliwa Jumamosi, kuwapa wakazi nafasi ya kupita kwa usalama kuepuka vita huko Kyiv, Sumy na mikoa mingine.
Naibu Waziri Mkuu wa Ukraine Iryna Vereshchuk alisema katika hotuba yake, “Natumai kuwa siku itapita vyema, njia zote zilizopangwa zitakuwa wazi na Russia itatekeleza majukumu yake ya kusitisha mapigano.”
Russia imepanua vita vyake nchini Ukraine kwa kulenga maeneo huko magharibi mwa nchi na inaonekana kuwa majeshi yake yanajikusanya tena karibu na mji mkuu, Kyiv, wakati Marekani na washirika wake wanaongeza vikwazo dhidi ya Moscow.
Afisa mwandamizi wa jeshi la Marekani, aliyezungumza kwa sharti jina lake lisitajwe kwa ajili ya kujadili masuala ya kijasusi, alithibitisha kuwa Russia imeanza kulenga maeneo upande wa magharibi mwa Ukraine, wakishambulia viwanja vya ndege huko Lutsk na Ivano-Frankivsk Ijumaa, ikiwa sehemu ya rundo la makombora zaidi ya 800 yakipigwa tangu kuanza kwa uvamizi huo.
Wakati vifaa vya majeshi ya Russia kaskazini magharibi mwa Kyiv bado viko kiasi cha kilomita 15 kutoka katikati ya mji, vifaa hivyo vinavyosaidia majeshi ya Russia vinasogea karibu na mji huo, afisa huyo amesema.
“Tunatathmini kuwa Russia imeanza kuongeza harakati zake huko kuelekea Kyiv, hususan kutoka mashariki,” msemaji wa Pentagon John Kirby aliwaambia waandishi siku ya Ijumaa. Majeshi ya Ukraine yameendelea kujihami kwa “mbinu na kwa haraka” ambapo majeshi ya Russia yamekatishwa tamaa, kulingana na afisa mwandamizi wa wizara ya ulinzi ya Marekani.