Madaktari walivyoshirikiana mwanzo wa mlipuko wa COVID-19

FILE - Wafanyakazi wa afya wakiwa katika chumba cha watu mahututi katika hospitali ya Brescia, Itali Machi 19, 2020.

Janga la virusi vya corona lilipoanza kusambaa katika nchi mbali mbali za dunia kutokea China madaktari na waatalamu wa sayansi hawakuwa na uzoefu au ujuzi wa kupambana na ugonjwa huo. 

Basi katikati ya mkanganyiko wa siku hizo za awali madaktari ambao walikuwa mstari wa mbele walianza kuwasiliana na wenzao pamoja na wafanyakazi wa afya bila ya kujali uwezo wao wa lugha, katika juhudi za kujaribu kuokoa maisha ya wengine, limeripoti shirika la habari la AP.

Bila ya kuwa na maelezo ya kufuata wala hakuna muda wa kusubiri kupatikana utafiti juu ya janga hilo, tovuti ya video za YouTube ilikuwa chombo muhimu kuelezea uchunguzi unaopatikana na picha za vipimo vya X-ray zilikuwa zikimiminika katika mitandao ya Twitter na WhatsApp.

Wakati Stephen Donelson alipowasili katika Chuo Kikuu cha Texas katika kituo cha Tiba kilichopo Kusini magharibi katikati ya mwezi Machi, alimkuta Dkt Kristina Goff akiwa ni kati ya wale waliogeukia kile alichokiita “simulizi kutoka maeneo mengine ambayo yaliaathiriwa awali.”

Familia ya Donelson ilikuwa haijaondoka katika makazi yao kwa wiki mbili baada ya COVID-19 kuanza kuenea huko Texas, wakiwa na matumaini ya kumlinda aliyepokea kiungo kilichopandikizwa mwilini mwake.

Hata baada ya tahadhari hiyo, siku mmoja mkewe alimkuta hawezi kupumua, ngozi yake ikibadilika kuwa blu, na kuita huduma ya dharura 911.

Huko New York au Itali, ambako mahospitali yalikuwa yanaelemewa, Goff anafikiri Donelson hata asingeweza kukubaliwa kuwekwa katika mashine ya kusaidia kupumua iliyokuwa wakati huo ni kitu adimu.

Lakini katika mji wa Dallas, “tulimsaidia kwa kila kitu ambacho kilikuwa katika uwezo wetu,” amesema.

Kama ilivyo kwa madaktari katika hospitali nyingine, Goff alikuwa mwanzoni mwa mtiririko wa kujifunza suala zito na lenye kukanganya.

“Ni mfano wa mafuriko ya tsunami. Jambo ambalo kama hujalipitia wewe mwenyewe, huwezi kulifahamu,” Daktari Pier Giorgio Villani nchini Itali amesema katika mfululizo wa mafundisho kadhaa aliyotoa jioni kupitia mtandao wa webinar kwa Jumanne sita mfululizo kutahadharisha vituo vingine vyenye kuhudumia watu mahututi kile ambacho watarajie.

Walianza kutoa maelekezo haya wiki mbili baada ya mgonjwa wa COVID-19 wa kwanza kufikishwa katika chumba cha mahututi hospitalini Itali na siku kumi kabla ya Donelson kuanza kuugua Texas.

Villani, anayefanya kazi katika mji wa Lodi ulioko kaskazini ameelezea juhudi za kuwapokea watu waliokuwa wakiongezeka mfululizo wakihitaji vifaa vya kuwasaidia kupumua.

Tulikuwa tunapokea wagonjwa 10, 12, 15 wanaohitaji kuwekewa mashine za kupumulia wakati tayari kitengo cha wagonjwa mahututi kilikuwa na wagonjwa 7 waliokuwa katika mashine za kusaidia kupumua.

Maelekezo yaliyokuwa yanatolewa kupitia picha za video, yalikuwa yameandaliwa na umoja wa vitengo vya kuhudumia wagonjwa mahututi ya Utaliana, GiViTi, na Taasisi isiyokuwa ya kibiashara Mario Negri Institute.

Baadae video hizo ziliwekwa katika mtandao wa YouTube, unakusanya simulizi za historia ya mlipuko wa janga la corona nchini Itali kama ulivyokuwa unaongezeka, ukielezewa na madaktari wa kwanza Ulaya kukabiliana na virusi vya corona.