Macron ateua Waziri Mkuu mpya kujitayarisha na uchaguzi ujao

Waziri Mkuu mpya wa Ufaransa Jean Castex

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amemteua Jean Castex, mtumishi muandamizi wa serikali na meya wa mji mdogo wa Ufaransa kuwa Waziri Mkuu mpya, wakati anafanya mageuzi makubwa katika baraza lake la mawaziri.

Castex aliyeongoza pia juhudi za kupambana na janga la COVID-19 anapewa jukumu la kuunda serikali mpya kulingana na taarifa kutoka ikulu hii leo.

Anachukua nafasi ya Waziri Mkuu Edouard Philippe, mwanasiasa mashuhuri kuliko rais Macron, aliyetangaza kujiuzulu mapema leo.

Waziri Mkuu mpya Castex anaetokea mrengo wa kulia na anachukua pia jukumu la kutayarisha sera mpya ya mageuzi ya kijamii, kiuchumi na mazingira kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022, hasa baada ya chama cha rais kushindwa kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa mwishoni mwa wiki iliyopita.

Rais Macron aliyepoteza umashuhuri wake anasema anataka kufufua upya malengo yake ya kuleta mageuzi baada ya kukabiliwa na upinzani mkubwa mnamo miaka mitatu ya utawala wake hasa kutokana na mageuzi yaliyokuwa na utata mfano suala la mafao lililozalisha vuguvugu la koti ya manjano.