Chakwera, mwenye umri wa miaka 65, alishinda kwa asilimia 58.57 ya kura katika uchaguzi uliofanyika Jumanne, ikiwa ni mabadiliko kwa matokeo ya uchaguzi wa awali mwezi Mei 2019, ambao ulifutwa na mahakama, Shirika la Habari la Uingereza Reuters limeripoti.
Kurejewa kwa uchaguzi kulionekana na wachambuzi kama ni jaribio la uwezo wa mahakama za Afrika kutatua suala la wizi wa kura na kudhibiti madaraka ya rais.
“Kusimama mbele yenu kama rais leo ni heshima kubwa. Ni heshima inayojaza furaha isiyosemeka na shukrani nyingi,” Chakwera alisema katika hotuba yake ya kukubali kuchukua madaraka.
“ Kwa msaada wenu, tutaweza kurejesha Imani ya kizazi kipya juu ya uwezekano wa kuwa na serikali ambayo inayowatumikia watu na siyo inayotawala,” aliuambia umati wa watu waliokuwa wakishangilia wakiwa wamevalia nguo za rangi ya bendera ya chama chake cha Malawi Congress Party (MCP) na muungano wa chama cha makamu rais Saulos Chilima.
MCP ni chama kikongwe nchini Malawi na ushindi wa Chakwera unakirejesha madarakani baada ya miaka 26 kikiwa cha upinzani.