Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 04:31

Rais mpya wa Burundi ateua baraza la mawaziri 15


Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye.
Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye.

Rais mpya wa Burundi Evariste Ndayishimiye Jumapili aliteua baraza jipya lenye jumla ya mawaziri 15, wanaume 10 na wanawake wa 5.

Baraza la zamani la mawaziri chini ya utawala wa hayati Rais Pierre Nkurunziza lilikuwa na mawaziri 21.

Kufuatia uteuzi huo, wizara ya usalama, mambo ya ndani na maendeleo ya jamii zimekwa pamoja na kuwa wizara moja, inayoongozwa na afisa wa ngazi ya juu katika polisi, Gervais Ndirakobuca.

Ndirakobuca alikua mkuu wa idara ya upelelezi chini ya uongozi wa hayati Nkurunziza.

Wizara ya mambo ya jumuiya ya afrika mashariki, vijana, michezo na utamuduni nazo pia zimejumuishwa pamoja na kuwa wizara moja inayoongozwa na aliyekua waziri wa mambo ya kigeni, Ezechiel Nibigira.

Wizara ya mambo ya nje sasa inaongozwa na aliyekua balozi wa Burundi kwenye umoja wa mataifa, Albert Shingiro huku wizara ya ulinzi, kwa mara nyingine ikiongozwa na raia.

Ni mara ya kwanza tangu mwaka wa 1976, kwa Burundi kuongozwa na rais ambaye ni jenerali wa jeshi, na waziri mkuu ambaye ni afisa mwenye cheo cha juu sana katika idara ya polisi ya taifa.

Waziri mkuu mpya Alain Guillaume Bunyoni yuko chini ya vikwazo vya marekani, kwa tuhuma za ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu, huku waziri mpya wa mambo ya ndani, usalama wa taifa na maendeleo ya jamii Gervais Ndirakobuca, akiwa amewekewa vikwazo na umoja wa ulaya, kwa tuhuma za uvunjanji mkubwa wa haki za binadamu, wakati wa maandamano ya kupinga muhula wa tatu wa rais Pierre Nkurunziza, mnamo mwezi April mwaka wa 2015.

Kipindi hicho Ndirakobuca alikuwa mkuu wa utawala katika afisi ya rais Nkurunziza.

Mawaziri wa zamani katika serekali ya hayati Nkurunziza ambao wameshikilia nyadhifa zao katika serekali mpya ni pamoja na waziri wa fedha, waziri wa elimu na utafiti wa sayansi, waziri wa afya na waziri wa kilimo na ufugaji.

Wengi wa mawaziri wapya ni kutoka chama tawala cha CNDD-FDD.

-Imetayarishwa na Patrick Nduwimana, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG