Maandamano maarufu dhidi ya utawala wa kijeshi wa Myanmar yalifanyika kwa siku ya tatu mfululizo Jumatatu, wiki moja baada ya serikali ya kijeshi kumweka kizuizini Aung San Suu Kyi na viongozi wengine wa serikali ya kiraia iliyochaguliwa.
Maelfu ya watu walijazana katika mitaa ya miji mikubwa ya Myanmar, ikiwa ni pamoja na mji mkuu, Naypyitaw, na jiji kuu la kibiashara la Yangon.
Waandamanaji hao walikuwa wamebeba mabango yanayosema Okoa Myanmar, tunataka demokrasia, pamoja na picha za Suu Kyi.
Polisi nao walitumia maji ya kuwasha kuwatawanya waandamanaji mjini Naypyitaw.
Maandamano hayo yaliingia katika awamu mpya Jumatatu wakati wafanyakazi wa umma, wafanyakazi wa reli, walimu na wafanyakazi katika sekta nyingine walipoanza mgomo wa kitaifa.