Maalim Seif adai dola imehusika kuihujumu CUF, ahamia ACT Wazalendo

Maalim Seif

Maalim Seif Shariff amesema Jumatatu anaridhia na maamuzi ya Mahakama Kuu kumtambua Ibrahim Lipumba, kuwa ndiye mwenyekiti wa Chama cha Wananchi CUF, anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa.

“Leo tumetangaza kujiondoa kwenye CUF tunajiunga rasmi na chama cha ACT Wazalendo,” amesema Maalim Seif. Ofisi zote za CUF tumezibadili na sasa zitapeperusha bendera za ACT,” ameongeza.

Uamuzi wa kujiunga na ACT

Maalim Seif amesisitiza kuwa ameamua kujiunga na ACT baada ya kugundua hujuma hiyo ya dola ya kuingilia mhimili wa mahakama.

Kiongozi huyo mkongwe katika siasa amesema kuwa: Tunaona CUF kama mzigo tumekwisha utua.”

Lakini amedai kuwa kuna ushahidi kwamba nguvu za dola kwa muongozo wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ilipanga mkakati wa mahakama kufanya uamuzi huu.

“Kesi hiyo (iliyoamuliwa) ina mkono wa dola, Hukumu iliyosomwa leo ilikuwa isomwe Februari 22, ikaahirishwa mpaka leo,” amesema Maalim Seif.

Mkakati wa kumsaidia Lipumba

Amesema huo ulikuwa mkakati wa kumpa nafasi Lipumba kwanza kubadilisha bodi yake ya uongozi, itambuliwe na pili kufanya mkutano wao feki, na hayo tayari yametekelezwa.

Maalim ametoa mfano wa amri ya mahakama ya Tanzania iliyotolewa kusitisha mkutano huo wa Lipumba, lakini jeshi la polisi lilikwenda kuulinda.

Serikali haikuheshimu amri ya mahakama

Ameuliza vipi tutasema dola haihusiki, iwapo hata amri ya mahakama haikuheshimiwa.

“Mahakama kwa maneno ni huru, lakini inaweza kutumika, namna nchi zetu zilivyo na usilinganishe mahakama za Marekani na Tanzania,

Amelalamika kuwa suala hili halikuanza leo, mkakati huu ulikuwepo siku nyingi.

Chama cha CCM amedai kuwa kimekuwa kikitumia ofisi za msajili wa vyama vya siasa, Rita na hata bunge, polisi , mahakama na vyombo vingine kuihujumu CUF.