Wizara ya Mambo ya Ndani ilitoa tangazo hilo kupitia akaunti ya Twitter takriban wiki tano baada ya kuamuru kufungwa kwa kambi za wakimbizi za Dadaab na Kakuma na kuipa UN wiki mbili kuwasilisha mpango wa kutekeleza agizo hili, vyanzo vya habari vimesema.
Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya na mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) Filippo Grandi walikutana Alhamisi mjini Nairobi na timu ya pamoja itaundwa kukamilisha na kutekeleza hatua za mpango wa kufunga kambi hizi, UN na serikali ya Kenya zimeeleza katika taarifa yao ya pamoja Alhamisi.
Kenya na UNHCR “zinakubaliana kuwa kambi za wakimbizi siyo suluhisho la muda mrefu kwa waliokoseshwa makazi yao” na wamedhamiria kushirikiana kutafuta ufumbuzi mbadala sambamba na Makubaliano ya Kimataifa juu ya Wakimbizi, taarifa hiyo imesema.
Moja kati ya kambi hizo mbili za wakimbizi huko kaskazini mwa Kenya, Dadaab, ambayo iko karibu na nyeti wa Somalia iliyogubikwa na vita, ilianzishwa mwaka 1991. Mwaka 2011, wakati ukame na machafuko yakiendelea Somalia, ilikuwa ni kambi kubwa kuliko zote duniani.
Tangazo la Alhamisi linaonyesha kuwa ni uamuzi wa mwisho wa Kenya baada ya miaka ya majadiliano juu ya kufungwa kwa Dadaab.
Mamlaka mjini Nairobi mara ya kwanza zilitangaza dhamira yao ya kufunga kambi ya Dadaab mwaka 2016, ikieleza wasiwasi wa usalama wa taifa kutokana na kujipenyeza kwa wanamgambo kutoka kikundi cha Kiislam cha al Shabaab chenye makao yake Somalia.
Uhusiano kati ya Kenya na Somalia umeendelea kuzorota sana katika mwaka uliopita tangu Mogadishu ilipositisha mahusiano ya kidiplomasia na Nairobi, ikiituhumu kuwa inaingilia kati masuala yake ya ndani.