Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 14:52

Kanisa Kenya lainasihi serikali kutofunga kambi za wakimbizi


Ramani ikionyesha kambi za Kakuma and Dadaab Kenya
Ramani ikionyesha kambi za Kakuma and Dadaab Kenya

Kanisa Katoliki nchini Kenya linaitaka serikali kusimamisha mpango wake wa kufunga kambi za wakimbizi za Dadaab na Kakuma na kuendelea kuwapa hifadhi wakimbizi hao.

Kanisa limesema wakimbizi hao zaidi ya 500,000 kutoka mataifa 15 wanaoishi nchini humo, itakuwa ni hatari kubwa kwa usalama wao endapo watarejea katika mataifa yao.

Ombi hili linatolewa siku chache baada ya mahakama nchini humo kusitisha utekelezaji wa agizo la serikali ya Rais Uhuru Kenyatta kutaka kuzifunga kambi hizo hadi kesi iliyowasilishwa mahakamani isikilizwe na kutolewa maamuzi.

Kanisa Katoliki linasema kufunga kambi za wakimbizi za Dadaab na Kakuma zilizo na zaidi ya watu 500,000 wanaohitaji hifadhi wakati huu wa janga la virusi vya Corona ni kuongeza matatizo mengine na hasa kwa taifa kama Kenya lililo katika makubaliano ya kimataifa kulinda haki za binadamu, kwani kufanya hivyo kutawaweka katika mateso na hatari isiyoweza kuepukika.

Muungano wa Maaskofu wa Kanisa hilo unaeleza, kupitia taarifa kwa vyombo vya habari, kuwa kwa sababu uamuzi wa Kenya kufunga kambi hizo ni kinyume cha sheria za kimataifa, serikali ya Rais Kenyatta haiwezi kufanya hivyo kwa sababu wanaotafuta hifadhi katika kambi za wakimbizi za Dadaab na Kakuma, hawafahamu iwapo nchi zao ni salama kurejea.

Askofu Mkuu Philip Anyolo, ameeleza katika taarifa yake, kuwa wakimbizi waliopo katika kambi hizo, hawawezi kuhakikishiwa usalama wa kutosha kwa sababu bado kuna mapigano na vitisho vingine vya usalama katika mataifa hayo.

Zaidi ya wiki mbili zilizopita, waziri wa usalama wa ndani nchini Kenya Fred Matiang’i ameeleza kuwa serikali ya Kenya inapania kufunga kambi hizo na kulitaka shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi UNHCR kutoa utaratibu wa kufunga kambi hizo haraka iwezekanavyo kwa kile serikali ilichokitaja kuwa ni “ukosefu wa usalama na changamoto za kiuchumi”

Bila ushahidi, Kenya imekuwa ikieleza kuwa mashambulizi ya kigaidi ambayo yamekuwa yakiripotiwa nchini mwake yanasadikiwa kupangwa na wanamgambo wa Al-Shabab wanaoaminika kupata himaya katika kambi za wakimbizi za Dadaab na Kakuma.

Hata hivyo, Kenya imekataa mpango wa UNHCR wa kufunga kambi hizo kwa utaratibu utakaochukua zaidi ya mwaka mmoja na badala yake kulitaka shirika hilo kuweka utaratibu wa haraka wa kufunga kambi hizo.

Shirika hilo limeeleza kuwa linafaa kupewa muda zaidi kuwahamisha wakimbizi wengine waliopo katika kambi za Dadaab na Kakuma katika nchi jirani kama vile Sudan Kusini na Ethiopia au hata Amerika na Canada, iwapo litalazimika kufanya hivyo.

Mahakama kuu nchini Kenya tayari imesitisha hatua za Kenya kufunga kambi hizo ikisubiriwa kusikilizwa kwa kesi inayopinga agizo hilo iliyowasilishwa na raia wa Kenya Peter Gichira anayetaka mahakama kufutilia mbali kauli ya kufungwa kwa sababu ya kile anachokitaja kuwa ni kinyume cha katiba ya Kenya.

Kenya imeonekana kughadhabishwa na jumuiya ya kimataifa hasa kwa kutounga mkono juhudi zake za kuliorodhesha kundi la Al-Shabab kuwa haramu na Umoja wa Mataifa, kwa madai kuwa kufanya hivyo ni kudidimiza harakati za kuwafikia waathirika wa machafuko nchini Somalia.

Kenya imekuwa ikiwapa makazi wakimbizi hawa kwa miaka 30 sasa na pametajwa kuwa makubaliano ya pande tatu yanayoihusisha Kenya, Somalia na UNHCR yamekuwa yakitekelezwa kwa mwendo wa kasi.

George Musamali, mfuatiliaji wa masuala ya usalama katika mataifa ya Pembe ya Afrika, anaeleza kuwa dhana ya Kenya kusema kuwa kambi hizi ni vitovu vya upangaji mashambulizi ya kigaidi hazina msingi.

Mnamo Novemba 2013, Mkataba wa pande tatu ulitiwa sahihi na serikali ya Kenya, Somalia na UNHCR kuanza kutekeleza utaratibu wa kuwarudisha kwa hiari wakimbizi nchini Somalia. Mnamo Desemba 8, 2014, kundi la kwanza lilikubali kurudi Somalia na mpaka sasa mchakato huo umewarejesha nyumbani raia wa Somalia wapatao 85,067.

Kenya na UNHCR zinatarajiwa kufanya mazungumzo mengine ya kufikia muafaka wa kufunga kambi hizo.

Imetayarishwa na mwandishi wetu, Kennedy Wandera, Nairobi, Kenya.

XS
SM
MD
LG