Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Januari 22, 2025 Local time: 18:52

Kenya kutatua mzozo wake na Somalia kwa njia ya kidiplomasia


Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta

Msemaji wa serikali ya Kenya Cyrus Oguna, ameambia waandishi wa habari kwamba Kenya haitachukua hatua kama ilizochukua Somalia na badala yake inasisitiza kufanyika mazungumzo.

Oguna amesema kwamba kenya haitawafukuza wanadiplomasia wa Somalia kama ilivyofanya Serikali ya Somalia kwa sababu hiyo itakuwa sawa na kulipiza kisasi.

Oguna amesema kwamba Kenya imekuwa nchi yenye ukarimu mkubwa sana kiasi cha kuwapa makao wakimbizi kutoka Somalia wanaoishi katika mojawapo ya kambi kubwa sana ya wakimbizi duniani ya Dadaab na Hagadera na kwamba juhudi zote zitachukuliwa kurudisha uhusiano mwema kati ya nchi hizo mbili.

Kenya inataka muungano wa IGAD na COMESA kuingilia kati na kusuluhisha mgogoro huo wa kidiplomasia.

“Sote tunajua kwamba Kenya na Somalia wana mambo mengi yanayofanana na maswala mengi yanayotuleta pamoja. Tuna historia inayotuunganisha, tuna ushirikiano wa kiuchumi na hata wa kijamii.” Amesema Oguna, akiongezea kwamba “Unajua pia kwamba tuna wanajeshi wetu wa KDF wanaolinda usalama Somalia kwa hivyo kuna mambo mengi sana yanayotuhusu ndani ya Somalia. Kuna pia swala la kidiplomasia na uhusiano wa kimataifa ambalo linahitaji ushikiano wa dhati. Nifanyie mema ili nami nikufanyie mema.”

Serikali ya Somalia ilitangaza kuvunja uhusiano wake wa kidiplomasia na Kenya jana jumatatu, na kuamurisha wanadiplomasia wake wote walio Nairobi kurudi Mogadishu huku wanadiplomasia wa Kenya walio Somalia wakitakiwa kuondoka ndani ya siku saba kuanzia leo.

Tangazo hilo lilitolewa na waziri wa habari wa Somalia Osman Abukar Dubbe kupitia televisheni ya taifa.

“Somalia imeamua kuvunja uhusiano wake na Kenya. Serikali inawaondoa wanadiplomasia wake wote kutoka Nairobi na kuamurisha wanadiplomasia wa Kenya walio Mogadishu kuondoka ndani ya siku saba kuanzia Desemba 15. Serikali ya Somalia imefanya uamuzi huo kutokana na kuingiliwa kisiasa na Kenya pamoja na hatua za kila mara za Kenya kuingilia uhuru wa Somalia.” Alisema Dubbe.

Hatua hiyo inajiri saa chache baada ya rais wa Kenya Uhuru Kenyatta kufanya mkutano na rais wa Somaliland, Muse Bihi.

Somaliland ilijitenga kutoka kwa Somalia mwaka 1991 na kujitangazia uhuru japo uhuru huo haujatambuliwa na umoja wa mataifa, Umoja wa Afrika AU, wala nchi yoyot ile.

Serikali ya Somalia inasisitiza kwamba Somaliland ni sehemu ya Somalia.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG