Kauli ya Trump juu ya chanjo, barakoa yakinzana na CDC

Robert Redfield

Siku hiyo ya Jumatano Mgombea urais wa chama cha Demokrati Joe Biden kwa upoande Wake alitangaza mipango yake ya kutoa chanjo pindi akishinda uchaguzi wa Novemba.

Akitoa ushahidi mbele ya kamati ya baraza la wawakilishi la bunge Mkurugenzi wa taasisi ya kudhibiti na kuzuia magonjwa CDC, Robert Redfield, amesema kutakuwepo na idadi ndogo ya chanjo ya kuzuia maambukizo ya virusi vya corona kati ya Novemba na Disemba mwaka 2020.

Lakini alisistiza kwamba chanjo hiyo haitiweza kupatikana kwa Wamarekani wote hadi baadae 2021.

Resfield anaeleza zaidi : "Ninadhani tunatajaria kua na za kutosha mwishoni mwa katyi kati ya mwaka au robô ya tatu mwaka 2021."

Saa chache baadae rais Trump akizungumza na waandishi habari juu ya hali ya ugonjwa wa Covid-19 hapa nchini alitoa maelezo tofauti na mtaalam wake.

Donald Trump alisema : Ninadhani alifanya makosa aliposema jambo hilo, sio habari sahihi. Na nilimpigia simu na hakuniambia jambo hilo na nina dhani amefahamu, huenda alibabaika, pengine ilielezwa vibaya. Tuko tayari kuaanza mara moja chanjo zikiwa tayari na huenda zikawa tayari mwezi Oktoba.

Jinsi serikali ya Marekani ilivyokabiliana na janga la corona imekuwa ni suala kuu katika uchaguzi wa urais wa mwezi wa Novemba na Trump amesema chanjo inaweza kuwa tayari siku ya uchaguzi.

Mbali na hayo Trump siku ya Jumatano alikinzana na maelezo ya mkurugenzi wa CDC kamba barakoa imedhihirisha kuwa ni kinga nzuri sana na huenda ikampatia mtu kinga zaidi kuliko chanjo.

Wakati wa mkutano ndani ya ukumbi na wapiga kura ambao hawajaamua watampigia kura nani ulioongozwa na George Stephanopoulos wa kipindi cha televisheni cha ABC News, Trump alisema virusi vya corona vitatoweka hata bila ya chanjo, akidai wananchi wa taifa hili watakuwa tayari na kinga ya mwilini.

Alikuwa akimaanisha kwamba wakati idadi kubwa ya watu wakishambuliwa na ugonjwa basi wananchi wengi wanakuwa na kinga dhidi ya ugonjwa huo.

Naye mpinzani wa Trump katika uchaguzi wa rais, Joe Biden akijaribu kutafautisha jinsi atakavyopambana na janga hilo hapo Jumatatno alitangaza mpango wake wa kutengeneza na kusambaza chanjo yenye nguvu akichaguliwa.

Akieleza juu ya mpango wake Biden alisema : "Ni mpango wenye ratiba kamili kuhusu lini wananchi watapata chanjo, ikifafanua wazi ni tabaka gani la raia watakaopewa chanjo kwanza, utaratibu maalum wa kusafirisha na kuhifadhi chanjo. Na nitatoa uongozi unaohitajika kutekeleza mpango.

Haya yote yanafanyika wakati Wamarekani wameshanaza kurudisha kwa posta kura zao kabla ya uchaguzi wa Novemba 3 na kulingana na uchunguzi wa karibuni wa maoni uliofanywa na ABC News na taasisi ya IPSOS unaonyesha asilimia 65 ya Wamarekani hawaridhiki na jinsi Trump anavyokabiliana na janga hili.