Idadi ya maambukizi Marekani imefikia zaidi ya watu 245,000, idadi kubwa zaidi kuliko nchi yoyote nyingine.
White House ya Marekani inatarajiwa Ijumaa kupendekeza watu wavae maski kuzuia kuenea kwa maambukizi ya virusi vya corona, baada ya hapo awali kusema maski hazikuwa muhimu katika kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo.
Wakati ulimwengu ukiendelea kukabiliana na janga la kuenea kwa virusi vya corona, sasa hivi maambukizi yamefikia milioni moja na elfu 30 na miaa 2 huku vifo vikikaribia elfu 55.
Licha ya kuongezeka kwa maambukizi hayo tayari watu 219,837 wamepona kwa mujibu wa mtandao wa kimataifa unaofutilia takwimu hizo wa Worldometer.
Dunia
Mataifa mbali mbali ya ulimwengu yameendelea kuchukua hatua madhubuti kutokana na kuongezeka kwa maambukizi baadhi zikiweka amri ya kubaki majumbani kwa wakati fulani huku nyingine zikisimamisha shuguli za kawaida kwa muda fulani.
Kenya
Tukianzia kwenye mataifa ya afrika mashariki waziri wa afya wa Kenya Mutahi Kagwe Ijumaa amelalamikia namna Wakenya wanavyochukulia suala la maambukizi kwa wepesi hata baada ya idadi ya maambukizi kuongezeka kutoka 81 hadi 110.
Amesema awali leo kwamba serikali inatafakari kuchukua hatua zaidi za kisheria hata baada ya kutangaza amri ya kutotoka majumbani saa za usiku iwapo watu hawatabadili mtazamo wao.
Uganda
Nchini Uganda malalamiko yameibuka miongoni mwa wakazi kwamba baadhi ya maafisa wa usalama wanashambulia watu majumbani mwao na kuwaibia kufuatia amri ya kutotoka majumbani kwa siku 14 iliotangazwa Jumatatu na Rais Museveni.
Amri hiyo imepelekea msemaji wa jeshi brigedia generali Richard Karemire kusema kuwa jeshi litashirikiana na polisi kuhakikisha amri ya rais inafuatwa huku maafisa wanao washambulia watu kukabiliana na nguvu za dola.
Tahadhari katika karibu kila nchi ya Afrika zimeendelea kuchukuliwa wakati maambukizi mapya yakiendelea kuripotiwa.
Marekani
Wakati huohuo Meya wa Jiji la New York Bill de Blasio tayari amependekeza wakazi wa New York kuvaa skafu, kitambaa au aina yoyote ya maski iliyotengenezwa kienyeji kufunika midomo na pua – lakini siyo maski maalum za tiba ya upasuaji. Amesema hizo zisitumiwe kwani ni kwa ajili ya wataalam wa afya.
Meya wa Los Angeles Eric Garcetti pia anawataka wananchi kufunika midomo wakiwa katika maeneo ya umma.
Dkt Fauci
Dkt Anthony Fauci, mtaalam wa ngazi ya juu wa magonjwa ya kuambukiza wa Marekani ambaye anaendelea kumshauri Rais Trump, ameiambia CNN Alhamisi usiku haelewi kwa nini baadhi ya majimbo ya Marekani hawajatoa amri ya kutotoka majumbani wakati nchi ikipambana na virusi vya corona.
Ukiangalia kile kinachoendelea nchini, sielewi kwa nini hatutoi amri ya kutotoka majumbani,” Fauci amesema.
Rais Trump
Trump amekataa kutoa amri ya kitaifa ya kutotoka majumbani, na kuacha uamuzi huo badala yake mikononi mwa majimbo, hata pale ambapo kunaongezeko la idadi ya vifo vinavyotokana na virusi hivyo.
Takriban majimbo 30 na Wilaya ya Columbia imeamuru wakazi wake kutotoka majumbani, na kusafiri tu pale panapokuwa na dharura.
Wauguzi walalamika Marekani
Mfumo wa huduma ya afya Marekani umeemewa na wingi wa wagonjwa wakati vifaa vya kuwahami wafanyakazi wa afya havitoshi. Wauguzi na madaktari wanaendelea kueleza vyombo vya habari juu ya hali za hospitali hizo.
Muuguzi mmoja amekiambia kituo cha habari cha ABC yeye na wafanyakazi wenzake wanahisi mfano wa “kondo kwenda machinjoni” wanapoelekea makazini.
Mwengine ameiambia kituo cha televisheni cha CNN kuwa hospitali anapofanya kazi imekataa kumpima iwapo ana maambukizi ya virusi vya corona. Amesema baadae alipimwa na rafiki yake katika hospitali hiyo na kuonekana na maambukizi. Muuguzi huyo anasema alikuwa akiwatibu wagonjwa wakati akijaribu kuomba apimwe.
Benki ya Dunia
Benki ya Dunia imepitisha takriban dola za Marekani bilioni 2 kwa ajili nchi 25 zilizo maskini zaidi duniani kupambana na janga la virusi vya corona.
India, Pakistan, Sri Lanka, Afghanistan na Ethiopia zitapata mgawo wa kwanza wa fedha hizo. Fedha hizo zimeelekezwa kwa ajili ya vifaa muhimu vya afya, ikiwemo maski na mashine za kusaidia kupumua.
India’s lockdown of more than 1 billion people has left hundreds of millions homeless and without food, prompting Prime Minister Narendra Modi to beg for their forgiveness.
URENO
Ureno imetangaza amri ya kusitisha kuwasili kwa ndege zote za kibiashara katika viwanja vyake vya ndege na raia wake hawataruhusiwa kutembelea miji mingine ila tu kwa shughuli za kikazi.
Amri hiyo mpya inaanza kutekelezwa April 9 na itaendelea kwa siku tano.
Serikali ya nchi hiyo imewasamehe wafungwa waliokuwa wamehukumiwa kifungo cha miaka 2 au chini ya hapo kudhibiti kuenea kwa virusi katika magereza.
Ureno ina wagonjwa wa corona waliopimwa chini ya 9,000.
Iraqi
Pia Alhamisi, madaktari watatu wa Iraq waliohusika na upimaji wa virusi vya corona wamesema nchi hiyo ina maelfu ya watu wenye maambukizi – zaidi ya hisabu ya watu iliyotolewa na maafisa wa serikali ya 772.
Wizara ya afya ya Iraq kwa kifupi imesema chanzo kinacho ripoti kile walichodai madaktari “sio sahihi.”
Kituo cha Kuleya Wazee
Huko mjini Seattle, Jimbo la Washington, maafisa wa serikali kuu wamependekeza kituo cha kuwaleya watu wazima kulipa faini ya dola za Marekani 611,000, ambapo watu 40 walikufa kutokana na virusi vya corona.
Kituo hicho kilikuwa ni chanzo cha maambukizi mapema mlipuko huo mwanzo ulipotokea Marekani.
Wasimamizi wa serikali kuu wanasema kituo hicho kilikuwa na matatizo kadhaa ikiwemo kushindwa kutambua na kuanza tiba sahihi ya wazee wakati ugonjwa wa kupumua ulipoanza na kujulikana kuwa ulisababishwa na virusi vya corona. Kituo hicho bado hakijatoa tamko lolote kuhusu faini hiyo.
Ujerumani
Nchini Ujerumani idadi ya maambukizi imefikia karibu 74,000 huku watu 872 wakiangamia kufikia sasa.
Hispania
Maambukizi nchini Uhispania tayari yamefika zaidi ya laki moja huku idadi ya vifo ikipita 4,000 kutokana na virusi hivyo.
Rashia
Rais wa Russia Vladmir Putin anasemekana kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi wakati taifa hilo likibuni App ya simu inayofuatilia mwenendo wa watu walioamuliwa kubaki kwenye karantini baada ya kugundulika na maambukizi.
Uturuki
Rais wa Utururuki Tayyip Erdogan amesema kuwa serikali yake inatadhmini kuchukua hatua madhubuti dhidi ya watu wanaokiuka masharti yaliowekwa kuhusiana na karantini.