Meya wa New York Bill de Blasio ameomba utawala wa Trump kupeleka msaada wa dharura katika mji huo mku wa biashara wa Marekani.
"Huu ndio wakati ambao tunalazimika kujitayarisha kwa wiki ijayo wakati tunatarajia kushuhudia idadi kubwa ya watu watakaoambukizwa na watakaofariki. Kile nilicho bayana wiki iliyopita, ni kuletewa madaktari na maafisa wa afya kutoka jeshi ili kutusaidia," amesema de Blasio.
Zaidi ya watu 3 700 wamefariki hapa Marekani tangu kulipuka kwa ugonjwa huo ikiwa idadi kubwa zaidi ya waliofariki China ambako janga hili lilianza.
Kulingana na Shirika la Afya Duniani, WHO, kufikia Jumanne jioni, zaidi ya watu 800,000 wamemabukizwa kote duniani na zaidi ya elfu 40 wamefariki kutokana na ugonjwa unaosababishwa na virusi hivyo vinavyo ambukiza kwa kasi kabisa.
Mkurugenzi wa kanda ya Pacific ya Magharibi ya WHO Takeshi Kasai, akizungumza na waandishi habari kupitia mtandao siku ya Jumanne, amsema, ingawa kuna mafanikio yanayopatikana huko Uchina na Korea Kusini, lakini janga linaendelea kwa haraka katika mataifa mengine na hivyo kuzitaka serikali za dunia kuimarisha juhudi za kupunguza kasi za mambukizi.
"Hatujui ni wka muda gani tutaendelea kupambana na Covid 19. Kuna watu usiku na mchana wanaofanya kila wawezalo kupambana na janga hili lakini haimkiniki kwamba virusi vitatoweka wiki ijayo au miezi ijayo” amesema Dkt Takeshi.
Matamshi hayo yanatia wasi wasi kote duniani na hata kukatisha tamaa kwa wengi, ambapo Italy ilitangaza Jumanne kuwa siku ya maombolezi ya kitaifa na bendera kupeperushwa nusu mlingoti.
Meya wa mji wa Milan aliwaongoza wataliana kwa dua na kukaa kimya kwa dakika moja kuwaombea watu elfu 11 5691 walofariki hadi hivi sasa nchini humo.
Licha ya hayo makampuni ya kutengeneza dawa yanaanza majaribiio ya chanjo hivi sasa, huku watu wakitafuta tiba kwa haraka iwezekanavyo amesema Dkt Takesha
"Tunatambua kwamba hakuna kitu kimoja kitakacho wafaa kila mtu katika kutayarisha mikakati kupambana na dharura kama hii lakini tumegundua kuna mbinu zinazofanana katika nchi mbali mbali," amesema Dkt Takesha
Miongoni mwa mbinu hizo anasema, ni kufunga shughuli za miji yote na kuwataka watu kubaki majumbani, kuwapima watu mapema na kuimarisha huduma za afya za umaa.
Hata hivyo katika nchi nyingi za afrika ambako viongozi wametangaza amri kali katika kujaribu kudhibiti usambazaji, kuna watu wanaolalamika na kusema hawataweza kupata chakula cha kila siku.
Hayo yakiendelea makampuni mbali mbali duniani yamelazimika kuacha majukumu yao ya kawaida na kuanza kutengeneza vifaa vya afya, ikiwa ni pamoja na mashini ya kusaidia mtu kupumua, maski hadi nguo za wauguzi na madaktari.