Miongoni mwao ni wanawake kadhaa kutoka nchi za Afrika, wengi wao wameshinda changamoto kubwa za kiuchumi na kijamii kufika mjini Paris.
Kwa mara ya kwanza katika historia, Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC), ilisema imefanikisha lengo la usawa wa kijinsia kwenye uwanja wa mashindano katika Olimpiki ya mwaka huu.
Wanariadha wanawake, ambao hapo awali walikuwa sawa na asilimia 2 tu ya washindani wa Olimpiki, sasa leo wako katika idadi sawa na wanaume. Walikuwa ni asilimia 48 ya wanariadha wanawake katika michezo ya Olimpiki huko Tokyo miaka mitatu iliyopita, ambayo iliahirishwa kwa mwaka mmoja kutokana na virusi vya Covid.
Wanawake kadhaa kutoka Afrika ni miongoni mwa watakaoshindana. Esti Olivier akiwa mpiga makasia katika timu ya mitumbwi kutoka Afrika Kusini. Anashiriki michezo ya Olimpiki kwa mara ya kwanza baada ya kutoshiriki michezo ya Tokyo kutokana na matatizo ya afya ya kimwili na kiakili.
Olivier anaeleza: “Sasa nikujikita kwenye mashindano sio kuzidiwa na shauku kubwa inayosababishwa na Olimpiki, lakini kufurahia mafanikio madogo kwa kila hatua nitakayopiga. Zimebaki wiki mbili kabla ya kushindana na nina hakika muda wote mashindano yanavyokaribia, wasiwasi utaongezeka. Lakini kwa sasa ni kufurahia kufika Paris.”
Kuendesha mitumbwi kwa kasia sio mchezo maarufu barani Afrika. Hata hivyo, timu za mitumbwi kutoka Angola, Misri, Morocco, Nigeria, Afrika Kusini na Tunisia zitawakalisha bara hilo kwenye michezo ya Olimpiki.
Olivier anasema mazoezi ya mchezo huo ni magumu kwa wanawake: “Nimefanya safari hii peke yangu kwa kiasi kikubwa na kwa sababu kuna wanawake wachache wanaoshiriki katika mbio za mitumbwi nchini Afrika Kusini, siku zote imenilazimu kufanya mazoezi kati ya wanaume. Kwa hakika hiyo ni changamoto. Ukosefu wa msaada ni changamoto. Na kuhangaika tu na maisha binafsi na michezo, unajua, kwa sababu huwezi kuzingatia tu kuwa mwanariadha, lazima pia niwe mke.”
Licha ya hatua iliyopigwa na wanariadha wanawake, changamoto nyingi zinazokwamisha maendeleo ya wanawake katika michezo bado zipo, ikiwemo kutolipwa mshahara sawa na wanaume, ubaguzi, na mazingira duni ya mazoezi.
Mwanariadha wa mbio za kati mwenye umri wa miaka 25 Lilian Odira kutoka Kenya, ambaye anashiriki katika mbio za mita 800, anasema ilikuwa ni safari ndefu kufika Paris, lakini muhimu zaidi ilikuwa bidi.
Odira anasema kuwa: “Michezo ilinifungulia milango mingi. Imenipa ujasiri wa kuwa hivi nilivyo. Imenipa ujasiri wa kukemea udhalimu ninaoweza kuushuhudia wakati wowote. Imenipa fursa ya kuwa mfano mzuri kwa wasichana wanaotaka kufikia kitu muhimu katika maisha yao, kuwaonyesha kuwa hata kwamba ni suala tete katika wakati mgumu au majukumu mbali ambayo unapaswa kutekeleza, bado inawezekana kufikia ndoto yako. Ukijituma, inawezekana.”
Kando na kushinda medali, Odira anataka kuvunja rekodi ya muda wake bora wa dakika moja, sekunde 59.
Kenya imepeleka wanariadha wanawake 20 mjini Paris, inakuja na fasi ya pili baada ya Afrika Kusini ambayo ilipeleka wanawake 24.
Wanariadha wanawake walishinda medali 17 huko Tokyo miaka mitatu iliyopita, na wanatumai kupata medali zaidi nchini Ufaransa.