Idadi ya waliofariki kutokana na tetemeko la ardhi Haiti yafikia 1,297

Wagonjwa na ndugu zao nje ya hospitali iliyoharibiwa na tetemeko la ardhi mjini Les Cayes, Haiti Agosti 14, 2021. REUTERS/Ralph

Idadi ya waliokufa iliongezeka Jumapili hadi kufikia 1,297 baada ya tetemeko la ardhi kubwa kuathiri Haiti siku moja mapema.

Huduma ya Ulinzi wa Kiraia ya Haiti ilisema idadi ya watu waliojeruhiwa pia iliongezeka hadi 5,700. Hospitali zinajitahidi kukabiliana na wale ambao wamefika kupatiwa huduma.

Maafisa waliendelea kutafuta manusura baada ya tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 7.2 kwa vipimo vya rikta. Tetemeko lililotokea Jumamosi asubuhi.

Tetemeko hilo, ambalo liliharibu nyumba, barabara na madaraja kwenye peninsula ya kusini magharibi mwa nchi, lilisababisha maelfu ya watu kupoteza makazi yao.

Gari lililoharibiwa na tetemeko la ardhi Haiti.

Wakazi wengi huko Les Cayes, jiji la tatu kwa ukubwa nchini humo lenye idadi ya watu 90,000, walikaa nje usiku kucha, huku matetemeko madogo madogo ya ardhi yakiendelea kutikisa eneo hilo siku ya Jumapili.

Kituo cha Kitaifa cha Kimbunga Marekani kimesema mapema leo Jumatatu kwamba ndege za uchunguzi zimegundua kuwa Dhoruba ya Fred imepungua kasi kidogo, lakini inatarajiwa kusababisha mvua nyingi na dhoruba mbaya sana katika pwani ya Florida baadaye mchana.

Fred inaweza kuwa imepungua kasi ya kusonga mbele, lakini watabiri walionya juu ya uwezekano wa vimbunga na mawimbi ya kutishia maisha na kuongezeka kwa dhoruba.

Watabiri wa hali ya hewa walionya kwamba kimbunga kimoja au viwili vinaweza kutokea Jumatatu asubuhi kwenye ya pwani ya magharibi ya Florida na wakati wa asubuhi hadi mchana kutoka eneo la Florida kaskazini kuelekea kusini magharibi mwa Georgia na kusini mashariki mwa Alabama.

Mara tu kimbunga Fred kitakapoingia kinatarajiwa kudhoofika, Kituo chaKitaifa cha Kimbunga cha Kitaifa cha Marekani NHC kilisema.