Hong Kong : Kukamatwa kwa waandamanaji 44 kwazua ghasia

Polisi nchini Hong Kong awaelekezea bunduki waandamanaji, Julai 30, 2019. Baadhi ya waandamanaji wamekamatwa kwa sababu ya kuandamana. PIcha na Reuters.

Waandamanaji wanaotetea demokrasia nchini Hong Kong wamekabiliana na Polisi, Jumanne usiku, baada ya wenzao 44 kukamatwa na kufunguliwa mashtaka ya kuzua ghasia.

Hii ni mara ya kwanza mshtaka kama hayo kufunguliwa tangu maandamano yalipoanza mwezi Juni.

Polisi wametumia gesi ya kutoa machozi kuzuia vurugu na kuwatawanya waandamanaji waliojitokeza nje ya kituo cha polisi katika wilaya ya Kwai Chung.

Waandamanaji walijibu kwa kuwarushia polisi chupa za plastiki na miavuli.

Mapema Jumanne, waandamanaji walisababisha huduma za usafiri wa treni ya chini ya ardhi na kuwazuia wasafiri kutoka kwenye treni.

Usafiri wa treni ulicheleweshwa na hata kusitishwa kabisa katika baadhi ya vituo.

Imetayarishwa na mwandishi wetu, Washington, DC.