Rais Xi Jinping alikuwepo katika kumbukumbu hiyo ya kitaifa mjini Beijing pamoja na viongozi wengine wa China mbele ya bendera ya taifa, vyombo vya habari vya serikali vimeripoti.
Virusi vya corona mara ya kwanza viliibuka mwisho wa mwaka 2019 huko China katika jimbo la Hubei, na kuua watu zaidi ya 3,300.
Kumekuwapo na malumbano iwapo China imekuwa wazi kutoa takwimu za afya juu ya virusi hivyo na tarehe ambayo virusi hivyo viliibuka.
Wakati China ikionekana kuwa inarejea katika hali ya kawaida baada ya kuwepo athari za virusi hivyo, maradhi hayo ya kuambukiza yameenea ulimwenguni, huku kukiwa na hali ya kukata tamaa na vifo.
Idadi ya maambukizi inaendelea kuongezeka wakati zaidi ya maambukizi milioni 1 yakithibitishwa ulimwenguni na takriban vifo 60,000. Wataalam wa afya na serikali zinaendelea kuhangaika katika vita hivyo dhidi ya maradhi hayo.
Marekani hivi sasa ndio penye maambukizi mengi ya virusi hivyo na watu walioambukizwa ni zaidi ya 278,000, lakini serikali yake bado haijakubali kuchukua hatua za pamoja kupambana na ugonjwa huo. Badala yake Rais Donald Trump ameyaambia majimbo wajitegemee kupambana na hali hii ambayo wakati huduma za afya zimeelemewa kutokana na janga hili.
Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia maambukizi CDC kimependekeza kuwa watu wavae maski kwenye mdomo na puani hata zisizokuwa za tiba kuzuia kuenea kwa virusi vya corona, wiki kadhaa baada ya kuuhakikishia umma kuwa maski hazikuwa lazima. Hata hivyo Trump amesema yeye hatovaa.
Trump amesema haisawiri kwake kukaa katika ofisi yake ya Ikulu akiwa amevaa maski usoni. “Nivae maski usoni wakati nina wasalimia marais, mawaziri wakuu, madikteta, wafalme na malikia – sioni hilo kufanyika.”
Shirika la habari la Associated Press limeripoti kuwa baadhi ya mahitaji ya vifaa vya afya yaliyopelekwa na serikali kuu katika baadhi ya majimbo hayawezi kutumika kwa sababu kadhaa, ikiwemo maski zilizo haribika na mashine za kusaidia kupumua ambavyo havifanyi kazi.
Marekani na nchi nyingine wamegeukia masoko huria kuagiza vifaa vya afya na madawa kwa ajili ya wagonjwa na vifaa vya kujilinda wafanyakazi wa afya kutokana na maambukizi, wakishindana katika manunuzi kati yao na kusababisha bei kupanda juu zaidi.
Mwanasiasa wa Ufaransa ameiambia shirika la habari la AP kuwa ushindani wa manunuzi ya mahitaji ya afya umekuwa ni “hazina inayotafutwa ulimenguni kote.”
Mashirika ya kijamii yametahadharisha hali ya kusimama kwa shughuli takriban ulimwenguni kote iliyoletwa na virusi vya corona kuzuia maambukizi, kuna mambo mengine yakijamii yamejitokeza ikiwa ni pamoja na matukio ya unyanyasaji wa wanawake majumbani wakiwa na wale wenye kuwanyanyasa.
Pia mifumo ya masomo imehamia katika mitandao ya jamii lakini siyo wanafunzi wote wanayo teknolojia inayohitajika kushiriki, ikidhihirisha na jamii zilivyokuwa zimegawanywa kutokana na uwezo wao wa maisha.
Wachambuzi wanasema kiwango cha watu kujiua kinaweza kuongezeka kutokana na watu kujitenga na kukosa kazi na fedha kuliko sababishwa na vita dhidi ya virusi vya corona.