China yakasirishwa na hatua ya Trump kuunga mkono waandamanaji Hong Kong

Rais Donald Trump

Serikali ya China imemuita Alhamis balozi wa Marekani mjini Beijing, ikipinga vikali hatua ya Rais Donald Trump ya kusaini miswada ya haki za binadamu ikiunga mkono waandamanaji nchini Hong Kong.

Rais Trump Jumatano alitia saini miswada miwili tofauti inayounga mkono waandamanaji wanaounga mkono demokrasia huko Hong Kong, licha ya makubaliano ya biashara katika kuleta uwiano na vitisho kutoka Beijing.

Baraza la Wawakilishi na Baraza la Seneti hapa Marekani walipitisha miswada yote miwili wiki iliyopita kwa kauli moja.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Le Yucheng alimwambia balozi Terry Branstad hatua hiyo ni kitendo cha uingiliaji kati mkubwa wa masuala ya ndani ya China.

Ameeleza kuwa kitendo hicho ni ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa, ilieleza taarifa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje China.

Vyanzo vya habari vinaeleza kuwa sheria za haki za binaadamu na demokrasia za kimataifa zinataka kufanyike tathimini ya kila mwaka, kujua kama Hong Kong ina uhuru wa kutosha.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya China zinasema serikali ya nchi hiyo itachukua hatua kali - ikiishutumu Marekani kwa ''dhamiri mbaya.''

Trump anaendeleza mazungumzo na China ya kumaliza vita ya kibiashara kati yao.

Serikali ya Hong Kong pia imeeleza kuwa uamuzi wa Trump kusaini miswada yote miwili haiwezi kutatua hali inayoendelea Hong Kong.