Shirika la Associated Press limeripoti kuwa watu kadhaa walikamatwa na polisi walirusha mabomu ya machozi kila wakati ambako kulizuka vurugu kati ya polisi na waandamanaji.
Mishumaa iliwashwa na usiku wa maombi ulifanyika sehemu mbalimbali za jiji hilo Jumamosi kuomboleza kifo cha mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Hong Kong Chow Tsz-Lok, 22, aliyekuwa anasomea masuala ya sayansi na teknolojia, ambaye alifariki katika hospitali ya Kowloon Ijumaa, siku nne baada ya kuangu kutoka ghorofa moja juu kwenye eneo la kuegesha magari katika wilaya ya Kowloon.
Polisi walikuwa wanajaribu kuwaondosha waandamanaji kutoka katika eneo hilo na walitupa mabomu ya machozi kadhaa. Inasadikiwa kuwa Chow alikuwa mtu wa kwanza kufa kutokana na majeraha aliyopata katika kipindi cha miezi mitano ya mapambano na polisi wakati waandamanaji wakidai kuwepo serikali ya kidemokrasia na mabadiliko katika sera.
Rais wa chuo kikuu Wei Shyy ametaka uchunguzi huru na wa kina ufanyike kujua ni katika mazingira gani Chow aliaguka.
Shyy ameongeza kuwa polisi walieleza kwa nini gari la wagonjwa lilichelewa kuingia katika eneo hilo la kuegesha magari baada ya Chow kujeruhiwa.
Picha za video zinazotumwa kwenye jukwaa la wanafunzi wa chuo hicho akiwemo Shyy zinaonyesha kile kinachoelekea kuwa ni kitendo cha polisi kuzuia gari la wagonjwa kuingia eneo hilo.
Polisi wamekanusha tuhuma dhidi yao kwamba walizuia gari la wagonjwa au walimkimbiza Chow, na kusababisha apate majeraha. Polisi wanataka suala hilo lisikilizwe na jopo la wachunguzi wa serikali.
Msemaji wa jeshi la polisi Hong Kong Suzette Foo amewaambia waandishi wa habari polisi waliingia katika eneo la kuegesha magari saa saba usiku Novemba 4 kuwatawanya waandamanaji ambao walikuwa wanawatupia polisi hao vitu mbalimbali. Amesema maafisa wa polisi walikuja kufahamu Chow aliaguka na kuumia baada ya kuwaona wazima moto wakimpa huduma ya kwanza mwanafunzi huyo.
Jibu hilo la jeshi la polisi na mambo yenye kukang’anya juu maelezo yao yamewakasirisha wakazi wa jiji hilo.
Waandamanaji wameitisha mgomo wa pamoja utakaofanyika Jumatatu katika jiji lote la Hong Kong, wakitarajia kuhujumu jiji hilo la kibiashara kama walivyofanya Agosti 5.