Biden na Putin wakutana Geneva

Rais wa Marekani Joe Biden (Kulia) na Rais wa Russia Vladimir Putin wakisalimiana walipowasili kufanya mkutano huko Villa La Grange, Geneva, Switzerland Juni 16, 2021. Saul Loeb/Pool via REUTERS

Rais wa Marekani Joe Biden na Rais Vladimir Putin wa Russia wanakutana Jumatano mjini Geneva, wote wawili wakiwa na matarajio madogo ya kufikia makubaliano muhimu.

Maafisa wa Marekani na Russia wanasema mazungumzo yao yatadumu kati ya saa nne mpaka tano.

Viongozi hao wamekubaliana kukutana katika kikao cha ana kwa ana wakiwa pamoja na mawaziri wao wa mambo ya nje, Antony Blinken upande wa Marekani na Sergei Lavrov wa Russia.

Taarifa za pande mbili zinaeleza kuwa mazungumzo ya baadaye yatashirikisha kundi jingine pana.

Balozi wa Marekani huko Russia John Sullivan na yule wa Russia hapa Marekani Anatoly Antonov ambao walirudi katika nchi zao mapema mwaka 2021 kufuatia uhusiano mbaya kati ya nchi hizo mbili wanatarajiwa kushiriki mkutano huo mjini Geneva.