Biden atakwenda Ulaya Jumatano na amepanga kuhudhuria mkutano wa nchi saba zenye uchumi mkubwa duniani, G-7, na ushirika wa kijeshi wa NATO, na baadaye kukutana na kiongozi wa Russia mjini Geneva, Uswizi, tarehe 16 mwezi huu.
Mkutano huo unafanyika huku mgogoro mkubwa katika uhusiano baina ya nchi hizo mbili ukiendelea kwa miaka mingi, na mivutano kuhusu masuala kadhaa ikiwa ni pamoja na Marekani kuishutumu Russia kwa udukuzi wa kimitandao, uingiliaji wa uchaguzi na ukiukaji wa haki za binadamu.
Katika waraka uliochapishwa na gazeti la Washington Post Jumamosi, Biden ameahidi kuunga mkono kile anachokiita "ushirikiano wa kidemokrasia" wa Washington, wakati wa mizozo na vitisho vingi kutoka Moscow na Beijing.
"Tunasimama kidete kushughulikia changamoto za Russia kwa usalama wa Ulaya, tukianza na uchokozi wake huko Ukraine, na hakutakuwa na shaka juu ya azma ya Marekani kutetea maadili yetu ya kidemokrasia, ambayo hatuwezi kuyatenga na masilahi yetu," aliandika.
Tangu aingie madarakani Januari mwaka 2021, Biden ameongeza shinikizo kwa Kremlin, na maoni yake yaliyomfananisha Putin na "muuaji" yalikosolewa vikali na Moscow.