Rais wa Marekani Joe Biden ana wasiwasi juu ya taifa kugawanyika katika vikundi viwili kati ya waliopigwa chanjo na wale ambao hawakupiga chanjo.
“Sitaki kuiona nchi ambayo tayari imegawanyika sana kugawanyika katika njia mpya, kati ya mahali ambapo watu wanaishi bila hofu ya COVID, na mahali ambapo anguko linafika na kifo na magonjwa mabaya yanarudi”, Biden alisema hayo Jumatano akitangaza juhudi mpya za chanjo ya corona na vivutio.
Kupata chanjo sio kitendo cha mrengo wa kisiasa ameongeza Biden, akibainisha uzalishaji wa chanjo hizo ulifanyika chini ya uongozi wa marais kutoka pande zote mbili. “Tunahitaji kuwa Amerika moja ilioungana na bila hofu” aliongeza.
Biden ameweka lengo la kuchanja asilimia 70 ya watu wazima nchini Marekani na chanjo walau moja ifikapo Julai 4, wakati nchi hiyo itaadhimisha Siku yake ya Uhuru. Kiwango kwa sasa ni asilimia 63.
Pamoja na viwango vya chanjo ya COVID-19 kubaki, nyuma haswa katika jamii za wachache Biden anapendekeza chanjo katika mpango wa maduka, ambayo inajumuisha zaidi ya vinyozi wa mitaa na wasusi wa nywele 1000. Wasusi hao na vinyozi watahudhuria mafunzo mwezi huu kuhusu chanjo ya corona na kisha kutoa mafunzo katika vituo vyao.