Lukashenko alisema wanajeshi 70,000 wa Belarus na wengine wanaofikia 15,000 wa Russia wataunda Kikundi cha Jeshi jipya la Russia na Belarus.
Wizara ya Ulinzi ya Uingereza ilisema katika taarifa za kipelelezi hivi karibuni zilizobandikwa katika Twitter kuwa licha ya kuwepo kanda ya video iliyotolewa na maafisa wa Belarus kuonyesha kuwasili kwa majeshi ya Russia nchini Belarus, “hakuna uwezekano kuwa Russia kwa hakika ilipeleka idadi kubwa ya wanajeshi zaidi huko Belarus.”
Wizara hiyo imekadiria uwezo wa nchi zote Russia na Belarus kukusanya wanajeshi katika ujumbe wa Twitter: “ Russia haina uwezo wa kutoa idadi inayodaiwa ya wapiganaji waliokuwa tayari: vikosi vyake vina majukumu nchini Ukraine. Jeshi la Belarus haiwezekani kuwa na idadi wanajeshi inayohitajika kwa ajili ya kukabiliana na operesheni ngumu zaidi.”
Wizara hiyo ilisema tangazo la muungano wa majeshi ya Russia na Belarus “inawezekana ni jaribio la kuonyesha mshikamano uliopo kati ya Russia- Belarus na kuishawishi Ukraine kuelekeza majeshi yake ya ulinzi katika mpaka wa kaskazini.
Kadhalika siku ya Ijumaa, miji ya Ukraine ya Kharkiv na Zaporizhzhia yalikabiliwa na milipuko kadhaa, kulingana na ripoti ya Reuters. Zaporizhzhia ni eneo la kituo cha kinu cha nishati ya nyuklia cha Ukraine. Kiwango cha uharibifu kutokana na milipuko hiyo hakikuweza kufahamika mara moja.
Habari hii imechangiwa na taarifa za mashirika ya habari ya AP, AFP na Reuters.