Baraza la Usalama lakutana kujadili kuuwawa kwa Rais wa Haiti

Hayati Jovenel Moise

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, UN, linakutana Alhamisi katika kikao cha dharura kujadili hali nchini Haiti kufuatia kuuwawa kwa Rais Jovenel Moise Jumatano na hivyo kulitumbukiza taifa hilo la Amerika ya Kati katika mzozo mkubwa zaidi wa kisiasa.

Mkutano huo uliyoitishwa na Marekani an Mexico utafanyika kwa faragha wakati viongozi wa dunia wakiendelea kulaani mauaji hayo na Marekani kutoa wito wa uchaguzi kufanyika kwa haraka iwezekanavyo.

Rais Joe Biden sawa na viongozi wengine wa dunia wameeleza masikitiko na mshtuko wao kutokana na kuuwawa kwa Rais Moise, akieleza kwamba hali nchini Haiti inatia wasiwasi.

Rais Joe Biden

Mkuu wa Polisi wa nchi hiyo Leon Charles aliwaambia waandishi habari jana usiku kwamba watu wanne wanaodhaniwa ni kati ya walioshambulia nyumba ya rais wameuliwa na wawili wamekamatwa.

Waziri mkuu wa mpito Claude Joseph ametangaza amri ya dharura na mipaka ya nchi kufungwa ili kuwasaka waliohusika na mauaji yaliyofanyika Jumanne usiku kuamkia Jumatano.

Joseph, kaimu Waziri Mkuu wa Haiti, ameeleza : "Kila mtu, kutoka kila aina ya chama cha kisiasa, kutoka kila aina ya nadharia, kila mtu hapa nchini ameshtushwa, kwa sababu kwa ufupi hatukutegema jambo hilo hakuna aliyetegemea kitendo hiki cha kikatili kufanyika."

Wanajeshi na polisi wa usalama wa Haiti wanaendelea kufanya doria katika mji mkuu wa Port au Prince Alhamisi wakati wananchi walioshtushwa na kitendo hicho wakiendela kujiuliza nani aliyehusika na kwa nini hilo limefanyika.

Balozi Bocchit Edmond (Twitter)

Balozi wa Haiti mjini Washington Bocchit Edmond alisema mke wa Rais Martine yuko katika hali mahtuti baada ya kujeruhiwa na amesafirishwa hadi Miami hapa Marekani kwa matibabu.

Alitoa wito kwa jumuia ya kimataifa kuisaidia nchi yake kuwatafuta wauaji ambao anasema walijitambulisha kama maafisa wa idara ya Marekani ya kupambana na dawa za kulevya, DEA.

Balozi Edmond ameeleza kuwa : "Tuna hitaji kuwa na kikosi cha jeshi kwa vile nchi yetu ilianzishwa na wanajeshi. Ni muhimu sana kuwa na jeshi ili kuweza kulinda mipaka yetu, na hivyo kudhibiti vyema mipaka yetu. Kwa sababu haikubaliki kuwepo na makomando, makomando wa kigeni kuingia nchini kumuua rais na kuondoka bila ya wasiwasi.

Mkuu wa Polisi Charles anasema watu waliohusika na mauaji ya rais ni mamluki na watafikishwa mbele ya sheria wakipatikana.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Marekani Ned Price akizungumza kwenye mkutano wake wa kila siku na waandishi habari amesema Marekani inaungana na kaimu Waziri Mkuu kuwataka wananchi kuwa watulivu.

Ameongeza kuwa Marekani iko tayari kuisiaidia nchi hiyo kwa kila aina ya msaada. Akisema ni muhimu pia kwa nchi hiyo kuandaa uchaguzi mwaka 2021 kuweza kutanzua matatizo ya kisiasa nchini humo.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani Ned Price

Msemaji huyo wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Marekani ameeleza : "Tunafahamu kwamba uchaguzi huru na haki ndiyo njia ya kidemokrasia kufikisha kikomo utawala wa muda mrefu wa utumiaji amri za utendaji na kurudisha mamlaka ya bunge ambao muda wake umemalizika."

Jumuia ya nchi za mabara ya Amerika, OAS, imeitisha mkutano wa dharura kujadili hali huko Haiti.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, amelaani mauaji na kutoa wito kwa Wahaiti kuendelea kuwa pamoja na kupinga kila aina ya ghasia. Naye mkuu wa masuala ya kigeni wa Umoja wa Ulaya Joseph Borrell ameonya juu ya hatari ya kuongezeka kwa ghasia na misukosuko ya kisiasa.

Vyanzo vya habari : AFP/ AP