Mgao mkubwa wa bajeti ya Uganda umepewa sekta za uzalishaji hasa kilimo, biashara, viwanda na utalii katika kile serikali inasema ni hatua ya kujikwamua kutokana na msukosuko wa kiuchumi unaosababishwa na janga la corona.
Bajeti hiyo ya Uganda inawapa afueni wafanyabiashara kwa kusamehewa kulipa ushuru ili kujiimarisha kutokana na janga la Corona.
Mashirika madogo madogo pia yamesamehewa kulipa ushuru sawa na wafanyakazi ambao hawatatozwa kodi kwa mshahara wao hadi kufikia mwezi Septemba 2020.
Lakini bajeti hiyo inaonyesha ushuru utakaotozwa kwenye bidhaa zinazoagizwa kutoka nje ya nchi umeongezwa, katika hatua ya kuimarisha uzalishaji ndani ya Uganda.
Waziri wa Fedha wa Uganda Matia Kasaija anatema :"Kwa kuzingatia majanga ambayo tumekumbana nayo katika siku za hivi karibuni, serikali imelegeza baadhi ya ushuru kwa kujali hali ya maisha ilivo kwa sasa, ili kusaidia uchumi kufufuka na kukua kwa kasi."
Ameeleza kuwa sekta za kilimo, utalii, uchukuzi, ujenzi na viwanda, ambazo zimeathirika zaidi kutokana na janga la virusi vya corona, nazo zimepata msamaha wa ushuru ili kuziwezesha kujikwamua upya na na kukua kwa haraka.
Kampuni zinazodaiwa ushuru na serikali, deni wanalodaiwa halitazalisha riba na kampuni zitasaidiwa katika uzalishaji ili kubuni nafasi kadhaa za ajira. Amos Wekesa ni mwekezaji katika sekta ya utalii, ameongeza.
Waziri Kasaija anaeleza : "Kulipa ushuru ni jukumu ambalo hatuwezi kuepuka. Tunahitaji ushuru wako hasa nyinyi wafanyabiashara ili tuwatengenezee mazingira mazuri ya kufanya biashara zenu na kupata faida nzuri zaidi."
Bajeti ya Uganda vile vile imetoa nafasi kwa benki za Uganda kuratibu upya mikopo iliyokuwa imetolewa kwa wafanyabiashara na watu binafsi ili kuweka mazingira mepesi ya kulipa mikopo hiyo, kwa kuzingatia kuyumba kwa soko la fedha kote duniani.
Benki kuu ya Uganda imepewa jukumu la kuhakikisha kwamba ada zinazotozwa kwa wanaotuma na kupokea pesa kwa kutumia simu, sawa na kulipia ada zao kwa kutumia kadi za benki, zinapunguzwa kabisa, ili kuzuia watu kubeba pesa taslimu, ikiwa mojawapo ya mikakati ya kupunguza maambukizi ya virusi vya Corona kwa watu kupokezana pesa.
Kwa wachambuzi wa maswala ya uchumi wa Uganda na wafanyabiashara kama Kapteni Francis Babu, bajeti ya nchi hiyo inaleta matumaini makubwa licha ya kuwepo janga la Corona.
Kapteni Francis Babu : "Uganda inapanga kufadhili bajeti yake kwa asilimia 72.5 huku ikikopa kiasi cha asilimia 27.5 ya shilingi trilioni 45.5 zinazohitajika. Bajeti hiyo ambayo tayari imejadiliwa na kupitishwa na bunge, inaanza kutekelezwa July 1 mwaka huu."
Imetayarishwa na mwandishi wetu, Kennes Bwire, Washington, DC.