Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 04:17

Uganda na Rwanda zasaini makubaliano ya kubadilishana watuhumiwa


Rais Paul Kagame and Rais Yoweri Museveni
Rais Paul Kagame and Rais Yoweri Museveni

Rwanda na Uganda zimesaini Ijumaa makubaliano ya kubadilishana watu wanaotuhumiwa kwa makosa kati yao na kuendelea na mchakato wa kuwaachia huru wafungwa na hatimaye kufunguliwa mipaka.

Makubaliano hayo ya kisheria yanayo zihusisha nchi za Uganda na Rwanda yatasimamia kesi zote za kisheria zikiwemo zile za vitendo vya uasi vinavyoendeshwa na raia wao katika nchi mwenza.

Marais wa nchi hizo mbili Yoweri Museveni wa Uganda na Paul Kagame wa Rwanda wameeleza kumekuwa na mafanikio tangu walipokutana juu ya ahadi ya pande mbili kufanya kila wanaloweza kuondoa mvutano kati yao.

Taarifa hiyo inaeleza : "Kwa hivyo, hatua ya kuachiwa kwa wafungwa kutoka pande zote mbili na dhamana ya kuendelea na mchakato huo kwa kufuata sheria na sheria za kibinadamu za kimataifa zimepokelewa vema."

Mkutano huo wa nne wa Marais wa Rwanda, Uganda, Angola na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo umefanyika katika mpaka wa pamoja wa mji wa Gatuna/Katuna. Makubaliano ya Luanda yamesimamiwa na Angola na DRC.

Makubaliano yaliyofikiwa kati ya nchi hizo yanapendekeza kuwa Uganda katika kipindi cha mwezi mmoja, ifanye uhakiki wa madai yote ya Rwanda juu ya vitendo vya uadui vinavyo fanywa na waasi walioko Uganda dhidi ya serikali ya Rwanda.

Serikali ya Uganda imekubali kuchukua hatua kabambe kuzuia mashambulizi hayo iwapo itathibitisha madai hayo ya Rwanda ni kweli na kuzuia yasitokee tena. Hatua hii kwa mujibu wa tamko la mkutano ni lazima ithibitishwe na kamisheni ya mawaziri ya muda kwa kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa mjini Luanda.

Baada ya kutekelezwa mapendekezo haya na kuripotiwa kwa viongozi wa nchi, wasimamizi hao wa makubaliano hayo watakutana katika siku 15 katika mkutano wa marais utakaofanyika Gatuna/Katuna kwa ajili ya ufunguzi wa mipaka na hatimaye kurejesha mahusiano kati ya nchi hizo mbili.

Kwa mujibu wa mwandishi wa Sauti ya Amerika Rwanda na Uganda zimeahidi kuzidi kutekeleza vipengele vya mkataba wa amani wa Luanda.

XS
SM
MD
LG