Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 18:38

Kagame: Sitashurutishwa kufungua mpaka na Uganda


Rais Paul Kagame wa Rwanda.
Rais Paul Kagame wa Rwanda.

Rais wa Rwanda Paul Kagame, alisema Jumatano kwamba serikali yake itafungua mpaka na Uganda wakati itajihisi kufanya hivyo akisisitiza kwamba hakuna mtu wala nchi yoyote itamshurutisha kufanya hivyo. 

Akihutubia mabalozi katika mkutano wa kila mwaka na waakilishi wa nchi za nje pamoja na mashirika ya kimataifa katika ikulu ya raia mjini Kigali, Kagame alizungumzia swala la Uganda na Rwanda, akigusia kwamba maafisa wake wanajitayarisha kwa mkutano wa Angola kuzungumzia uhusiano kati ya nchi hizo mbili.

Hata hivyo, rais huyo alisisitiza kwamba hakuna litakalobadilika iwapo matakwa ya Rwanda hayatazingatiwa.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ikulu ya rais mjini Kigali, iliyowekwa kwenye ukurasa wa twitter wa serikali ya Rwanda, rais Kagame amesema mgogoro wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili, ni jirani wake Uganda akielezea kwamba tatizo lililopo ni kubwa kuliko kufungwa kwa mpaka kama inavyoripotiwa.

“Hata iwapo tunafungua mpaka wa Rwanda na Uganda, swala kuu ni kukamatwa na kuzuiliwa kwa raia wetu nchini Uganda”, amesema rais Kagame.

Rais wa Rwanda Paul Kagame na rais wa Uganda Yoweri Museveni
Rais wa Rwanda Paul Kagame na rais wa Uganda Yoweri Museveni

Mwezi Desemba mwaka uliopita 2019, Uganda iliachilia huru raia kadhaa wa Rwanda, waliokuwa wanazuiliwa kwa maadai ya kuifanyia Rwanda ujasusi.

“Swala hili sio la kufunga wala kufungua mpaka. Ni swala la raia wetu kukamatwa wakiwa Uganda. Tumefunga mpaka kwa sababu hatutaki raia wetu kuingia Uganda kwa sababu watakamatwa. Lakini raia wa Uganda wapo huru kuingia Rwanda”, aliendelea kusema rais Kagame.

Uganda imekuwa ikikanusha madai ya kuakamata raia wa Rwanda wanaotii sheria, ikisisitiza kwamba wanaokamatwa wanashukiwa kufanya uhalifu.

Kagame alitaja hatua ya Uganda ya kuachilia huru raia wa Rwanda kuwa nzuri lakini akawa mwepesi wa kuongezea kwamba haitoshi na kwamba ni idadi ndogo sana ya raia wa Rwanda waliachiliwa huru, akidai kwamba raia wawili wa Rwanda walikufa wakiwa kizuizini Uganda kutokana na mateso.

Kagame pia alisema kuongoza jumuiya ya Afrika mashariki ni kazi ngumu sana kuliko kuongoza umoja wa Afrika – AU.

“Na wakati haya yote yanaendelea, tunazungumza sana kuhusu ushirikiano katika jumuiya ya Afrika mashariki. Tutaendelea tu kuzungumza kuhusu ushirikiano huo bila mafanikio kama tunayofanya ni tofauti na tunayosema. Tunastahili kufanya yaliyo sawa”, aliendelea kusema Kagame.

Rwanda inaishutumu Uganda kwa kuunga mkono makundi ya wapiganaji yenye lengo la kupindua serikali ya Kagame, kuwakamata raia wa Rwanda, na kuhujumu uchumi wake.

Rwanda imeweka marufuku ya biashara na kufunga mpaka wake na Uganda tangu Februari mwaka uliopita 2019 na kuwaonya raia wake kutoingia Uganda.

Uganda nayo inaishutumu Rwanda kwa kuiwekea marufuku ya kibiashara, kufanya upelelezi dhidi ya serikali ya rais Yoweri Museveni kwa lengo la kutatiza usalama wake, kuwafuta kazi maafisa wa ngazi ya juu raia wa Uganda waliokuwa wakifanya kazi Rwanda na kueneza habari za chuki dhidi ya Uganda na maafisa wake serikalini.

Rwanda imekuwa na uhusiano mbaya na majirani wake Burundi na Uganda, huku Burundi ikiishutumu kwa kuyapatia silaha makundi yanayopinga utawala wa rais Piere Nkurunziza na kupanga njama za kuangusha utawala wake katika mapinduzi yaliyofeli ya mwaka 2015.

Uganda imekataa kuzungumzia mgogoro wake na Rwanda katika vyombo vya habari.

Imetayarishwa na Kennes Bwire – VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG