Mamia ya maafisa wa polisi wa Kenya wawasili Haiti

Ndege ya Shirika la ndege la Kenya ilipotua katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Toussaint Louverture ikiwa na majeshi ya usalama wa Kenya Juni 25, 2024.

Mamia kadhaa ya maafisa wa polisi kutoka Kenya waliwasili katika mji mkuu Port-au-Prince, ambapo uwanja mkuu wa ndege wa kimataifa ulifunguliwa tena mwisho wa mwezi Mei baada ya ghasia za magenge kulazimisha kufungwa kwa takriban miezi mitatu.

Haikufahamika mara moja kazi ya kwanza ya Wakenya itahusu nini, lakini watakabiliana na magenge yenye ghasia ambayo yanadhibiti asilimia 80 ya mji mkuu wa Haiti na wamesababisha zaidi ya watu 580,000 kote nchini kukosa makazi huku wakivamia maeneo yaliyo jirani kwa utashi wao wa kudhibiti eneo kubwa zaidi.

Kuwasili kwa Wakenya kunakuwa ni tukio kubwa la nne la jeshi la kigeni kuingilia kati nchini Haiti. Wakati baadhi ya Wahaiti wamepokea kwa furaha kuwasili kwao, wengine wanaangalia kwa tahadhari kuwepo kikosi hicho, kwa kuwa walinda amani wa UN waliopelekwa mwaka 2004-2017, walikabiliwa na tuhuma za ubakaji na kuanza kwa ugonjwa wa kipindupindu.

Kutokana na habari za kuwasili kwa maafisa wa polisi wa Kenya, wakazi wa mji mkuu wa Haiti, Port Au Prince wamekuwa na maoni mchanganyiko kuhusu kuwasili kwa maafisa hao, baadhi wakihoji ikiwa kikosi hicho kitaweza kurudisha utulivu nchini mwao.

Mwalimu Verna Siber anaeleza: “Ni lazima maafisa zaidi waletwe. Wanahitaji kuwepo kila mahali hapa nchini ili watu waweze kuwa na uhuru.”

Muuguzi Nathalie Francois anasema: “Sio wageni ambao watatatua matatizo yetu. Ni juu yetu sisi kuja na suluhisho, hata hivyo, tunapokea msaada kwa sababu hatuwezi kwenda popote kwa kuwa maeneo mengi ya nchi hayana sheria.”

Polisi wa Kenya wataongoza kikosi maalumu cha kupambana na magenge yenye nguvu ambayo yamesababisha ghasia zilizopelekea mauaji mengi mwaka huu.

Jeshi la polisi la Haiti halina uwezo wa kutosha na lina ukosefu wa vifaa.

Ripoti ya Umoja wa Mataifa inaeleza kwamba ina karibu maafisa 4,000 walioko kazini wakati huu kwenye nchi yenye zaidi ya watu milioni 11.