Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 19:38

WHO yaripoti kasi mpya ya maambukizi ya COVID-19


Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus
Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus

Shirika la Afya Duniani (WHO) Jumapili limeripoti kuongezeka kwa maambukizi mapya 183,000 ya COVID-19, ongezeko kubwa kuliko yote kwa siku moja ambayo imerekodi tangu kuanza kwa janga hilo.

Maafisa wa WHO wamesema kwa wiki kadhaa ufuatiliaji wa mlipuko huo umeangazia mabara ya Marekani, na idadi ya Jumapili imeonyesha ongezeko la siku moja la zaidi ya maambukizi 116,000 katika eneo Latin Amerika na Amerika ya Kaskazini.

Brazil ilikuwa inaongoza kwa takriban maambukizi mapya 55,000, ikifuatiwa na Marekani ikiwa na zaidi ya maambukizi 36,000 na India ikiwa takriban na maambukizi mapya 15,000.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema Jumatatu tishio kubwa hivi sasa sio virusi vyenyewe, lakini hasa “ ni ukosefu wa mshikamano wa kimataifa na uongozi.”

“Hatuwezi kulishinda janga hili wakati ulimwengu umegawanyika,” amesema.

Zaidi ya darzeni ya majimbo ya Marekani yameshuhudia kuongezeka kwa maambukizi. Dkt Tom Inglesby, mkurugenzi wa Kituo cha Usalama wa Afya katika Chuo cha Afya ya Jamii cha Johns Hopkins Bloomberg, amesema kupitia kipindi cha “Fox News Sunday” kwamba kuongezeka kwa maambukizi kunatokana na mchanganyiko wa kuongezeka kwa upimaji na mlipuko hasa wa maambukizi.

“Unaweza kupambanua kati ya kuongezeka upimaji na hali ya dharura ya ugonjwa huu kwa kuangalia kiwango cha watu wanaolazwa hospitali, kiwango cha watu walioko kitengo cha mahututi, na asilimia ya jumla ya wale wanaogundulika kuwa na maambukizi katika jimbo mojawapo,” Inglesby amesema.

“Na katika majimbo mengi, katika yale ulioonyesha, hususan Arizona, Texas, Carolinas, Florida, kile tunacho shuhudia ni kuongezeka maambukizi kwa waliopimwa na wengi wao kulazwa hospitalini, hali ya wagonjwa ikiwa mbaya.”

Rais Donald Trump amerejea kusema anaamini idadi ya maambukizi yaliothibitishwa nchini Marekani, ambayo inaongoza duniani kukiwa na zaidi ya maambukizi milioni 2.2, ni kutokana na juhudi katika nchi hii kufanya upimaji.

“Upimaji wetu wa virusi vya corona ni wa juu zaidi (vipimo 25 milioni) na ambavyo vya utaalam wa juu, na inatufanya tuonekane kama tuna maambukizi mengi zaidi, hasa ukilinganisha na nchi nyingine,” alituma ujumbe wa tweet Jumapili jioni.

Hilo lilifuatia maoni yake aliotoa katika mkutano wa hadhara wa kampeni Jumamosi ambapo rais alisema : “Unapofanya vipimo kwa kiwango hicho, lazima utajikuta una maambukizi zaidi. Hivyo, nawaambia watu wangu, “Punguzeni kasi ya upimaji.”

White House baadae ilisema kuwa rais alikuwa anafanya mashara.

Wajumbe wa kikosi kazi cha virusi vya corona cha White House wamepangiwa kutoa ushuhuda mbele ya kamati ya Nishati na Biashara ya Baraza la Wawakilishi Jumanne, na Spika wa Baraza la Wawakilishi Nancy Pelosi amesema, “Wananchi wa Marekani wanahitaji majibu kwa nini Rais Trump anataka upimaji upunguzwe kasi wakati wataalam wanasema upimaji zaidi unahitajika.”

“Juhudi za Rais kupunguza kasi ambapo upimaji unahitajika kwa dharura, kuficha ukweli wa kiwango cha maambukizi ya virusi inamaanisha Wamarekani zaidi watapoteza maisha yao,” amesema Pelosi katika tamko lake Jumapili.

XS
SM
MD
LG