Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 24, 2024 Local time: 06:03

Obama akosoa uongozi wa Marekani unavyoshughulikia janga la corona


Rais mstaafu Barack Obama akiwahutubia wahitimu wa Shule za Sekondari Marekani kupitia mitandao ya jamii ikiwa ni njia mbadala ya utamaduni wa sherehe za kumaliza masomo,Mei 16, 2020. (Foto: Reuters)
Rais mstaafu Barack Obama akiwahutubia wahitimu wa Shule za Sekondari Marekani kupitia mitandao ya jamii ikiwa ni njia mbadala ya utamaduni wa sherehe za kumaliza masomo,Mei 16, 2020. (Foto: Reuters)

Rais mstaafu wa Marekani Barack Obama Jumamosi alitoa hotuba mbili kwa njia ya mtandao – ya kwanza ni mahafali ya wahitimu wa vyuo vya kihistoria vilivyoasisiwa na watu weusi maarufu kama HBCU na nyingine kwa wahitimu wa mwaka 2020 wa shule za sekondari.

Mahafali hizo mbili zilionyeshwa mubashara kupitia mitandao ya YouTube, Facebook na Twitter kwa sababu ya amri ya kutotoka nje iliosababishwa na janga la virusi vya corona lilioko duniani na kufanyika kama njia mbadala ya utamaduni wa sherehe za kumaliza masomo.

Pamoja na hongera za kawaida ambazo zinatolewa kwa wahitimu wakati kama huu, Obama alikosoa uongozi wa Marekani ulioko madarakani, jambo ambalo rais huyo mstaafu amekuwa akijizuia kufanya.

Obama alizungumzia janga la corona na jinsi lilivyodhihirisha ukosefu wa usawa nchini Marekani. Pia ameukosoa uongozi wa Marekani jinsi unavyolishughulikia janga hilo, bila ya kumtaja Rais Donald Trump.

Obama amewaambia wahitimu hao “itawabidi mkuwe kwa haraka kuliko baadhi ya vizazi vilivyopita. Janga hili limetikisa mwenendo wa kawaida na imedhihirisha wazi matatizo mengi yaliyojikita katika nchi yetu – kuanzia kukosekana usawa kiuchumi hadi matabaka ya kikabila na ukosefu wa huduma ya msingi ya afya kwa watu wanaohitajia. Imewazindua vijana wengi juu ya ukweli wa kuwa njia za kizamani za kuendesha mambo hazifanyi kazi; na kuwa haijalishi ni kiwango gani cha fedha unapata iwapo kila mtu anayekuzunguka ana njaa na anaumwa; na kuwa jamii yetu na demokrasia yetu inafanya kazi pale tu tunapokuwa hatujifikirii sisi wenyewe tu, lakini kuhusu kila mmoja wetu.”

Aliongeza kusema, janga hili “limeondoa pazia” kuhusu “ukweli thabiti” na kwamba “ni kitu ambacho sote hatimaye lazima tuukubali mara tu utoto wetu unapofikia kikomo. Wazee wote wale ambao mlikuwa mnafikiria ndio wasimamizi na wanajua kile wanachokifanya? Imedhihirika hawana majibu yote. Wengi wao hata hawaulizi maswali sahihi. Kwa hiyo kama ulimwengu utakuwa na hali bora zaidi, itakuwa ni jukumu lenu.

Aliwatahadharisha wahitimu hao dhidi ya “kufanya mambo yanayo wapendeza, na yale yaliyo rahisi – hivyo ndivyo watoto wadogo wanavyofikiria. Kwa bahati mbaya wale wanaoitwa watu wazima, wakiwemo baadhi na vyeo vya kuvutia na kazi muhimu, bado wanafikra kama hizo za kitoto --- na ndiyo sababu mambo yameharibika.”

Obama amesema anatarajia kuwa kila mhitimu badala yake “atajikita katika maadili yenye kudumu, kama vile ukweli, uchapaji kazi, kuwajibika, uadilifu, ukarimu, na kuheshimu wengine. Sio kwamba mtapatia kila wakati, mtafanya makosa kama vile sote tunavyokosea. Lakini mkisikiliza ukweli ulioko ndani ya nafsi zenu, hata kama ni jambo gumu, hata kama halikupendezi, watu watatambua. Wataegemea kwenu nyinyi. Nyinyi mtakuwa ni sehemu ya suluhisho badala ya kuwa sehemu ya tatizo."

Akiongea na wahitimu hao wa vyuo ambavyo kihistoria viliasisiwa na watu weusi Obama amesema, “Hebu tuweni wakweli, ugonjwa kama huu [COVID-19] inadhihirisha masuala ya ndani ya kukosekana usawa na majukumu zaidi yanayo wakabili jamii za watu weusi ambayo historia inatuonyesha namna walivyokabiliana nayo katika nchi hii.

Rais huyo mstaafu alisema, “Tunashuhudia kukosekana uwiano wa athari ya COVID-19 katika jamii zetu, kama vile tunavyoshuhudia pale mtu mweusi anapotoka kufanya mazoezi ya kukimbia na baadhi ya watu wanahisi wanaweza kumsimamisha, kumhoji na kumtupia risasi iwapo hatasimama kujibu maswali yao,” akifanya rejea ya tukio la Ahmaud Arbery, Mtu mweusi wa miaka 25 aliyepigwa risasi wakati akifanya mazoezi huko Georgia.

XS
SM
MD
LG