Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Novemba 23, 2024 Local time: 03:32

Kenya yafunga mipaka yake na Tanzania, Somalia


Rais wa Tanzania, John Magufuli, na mwezake wa Kenya, Uhuru Kenyatta.
Rais wa Tanzania, John Magufuli, na mwezake wa Kenya, Uhuru Kenyatta.

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta, Jumamosi alitangaza kufungwa kwa mipaka kati ya nchi hiyo na majirani wake, Tanzania na Somalia, katika kile alichokiita "juhudi zaidi za kukabiliana na kuenea kwa virusi vya Corona."

Katika hotuba iliyorushwa moja kwa moja na vyombo vya habari kutoka Ikulu ya Nairobi, Kenyatta alisema ni marufuku kwa watu kutoka au kuingia Kenya kupitia mipaka hiyo.

"Kuingia au kutoka nchini Kenya, ikiwa ni pamoja na magari ya abiria, sasa ni marufuku," alisema Kenyatta.

Hata hivyo, rais huyo alisema magari ya mizigo bado yataendelea kuruhusiwa kuingia na kutoka "lakini ni lazima madereva wawe wamefanyiwa vipimo na kubaini kwamba hawana virusi vya Corona."

Katika siku za karibuni serikali ya Kenya imesema kumekuwa na ongezeko kubwa la maambukizi kutokana na kutofuatwa kwa kanuni zilizowekwa kupambana na ugonjwa huo kwenye mipaka yanke na nchi jirani.

Kenyatta inakitaja kuwa uingizaji wa maambukizi ya kiwango cha juu nchini mwake na hivyo basi kuwaweka raia wake katika hatari ya maambukizi ya virusi vya Corona.

Rais Kenyatta alieleza kuwa mipaka ya Kenya na nchi hizi mbili imeingiza maambukizi 43 ya virusi vya Corona ambayo ni robo ya visa 166 ilivyoripoti wiki jana na hivyo basi ipo haja ya dharura ya kuwazuia raia wa nchi hizo mbili kuingia mipaka yake.

Aliongeza kuwa maambukizi 14 ni ya watu walioingia Kenya kupitia Wajir, 16 kupitia mpaka wa Namanga, 10 kupitia Mpaka wa Isebania, 2 kupitia mpaka wa Lunga Lunga na mmoja kupitia mpaka wa Loitokitok.

Kenyatta vile vile alisema watu 78 waliopimwa na kupatikana na maambukizi ya virusi vya Corona kutoka nchi hizi mbili, wamerejeshwa nchini mwao kupata matibabu zaidi.

Mpaka kati ya Kenya na Tanzania unapitia miji ya Namanga, Loitokitok, Taveta-Holili, Isebania na Lunga Lunga.

Serikali ya Kenya imekuwa ikijikuna kichwa kutokana na maambukizi yanayoongezeka kila kuchao, huku visa kadhaa vikiripotiwa kutokea nchi jirani, hususan Tanzania na Somalia, na tayari imetangaza kuweka vituo vya maabara katika mpaka wake na Tanzania katika eneo la Namanga.

Kenya inatarajia kupunguza maambukizi zaidi ya virusi vya Corona kupitia madereva wa malori ya masafa marefu nchini mwake na kuwahakikisha usalama wa raia wake.

Baadhi ya madereva kwenye kituo cha mpaka kati ya Kenya na Tanzania, cha Namanga, wamekuwa wakilalamikia kile wanachokiita unyanyapaa.

Kenyatta aidha alitangaza kuongezwa kwa muda wa marufuku ya kutoka nje usiku kote nchini, na zuio la kutoka au kuingia kwenye kaunti za Nairobi, Mombasa, Kwale, Kilifi na Mandera.

-Mwandishi wa VOA Kennedy Wandera pia amechangia ripoti hii

XS
SM
MD
LG