Mkurugenzi Mtendaji wa IMF Kristalina Geogieva aliwambia mawaziri, maafisa wa Umoja wa Mataifa na wajumbe wengine wakati wa mkutano kupitia mawasiliano ya video Ijumaa kwamba bara la Afrika halina rasilmali na uwezo wa huduma za afya kushughulikia janga hilo.
Mkurugenzi huyo amesema ni wajibu wa taasisi hizo kuchukuwa hatua zinazostahili kuzisaidia nchi za Afrika kukabiliana na janga hilo.
Ameeleza kuwa bara hilo linahitaji angalau dola bilioni 114 kugharimia mahitaji yake ya dharura ya fedha.
Amesema bila shaka janga hilo litasababisha uchumi wa bara hilo kushuka kwa asilimia 1.25 mwaka 2020 ambacho ni kiwango kibaya kuwahi kushuhudiwa.
Hata baada ya ahadi za msaada kutoka wafadhili wa kikanda, binafsi na msaada wa nchi kwa nchi, Afrika bado inakabiliwa na pengo kubwa la karibu dola bilioni 44, wameeleza maafisa wa mashirika ya kimataifa ya fedha.
Mkutano huo wa “Mobilizing with Afrika” uliofanyika wakati wa mikutano ya majira ya vikao vya Benki kuu ya dunia na IMF.
Imetayarishwa na mwandishi wetu, Washington, DC.