Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Januari 22, 2025 Local time: 23:49

Maambukizi ya Corona yaongezeka barani Afrika


Mzee ajifunika mapua kama njia ya kujikinga kutokana na virusi vya Corona.
Mzee ajifunika mapua kama njia ya kujikinga kutokana na virusi vya Corona.

Idadi ya watu waliothibitishwa kuambukizwa virusi vya Corona barani Afrika iliendelea kuongezeka Alhamisi huku serikali zikiongeza juhudi za kuzuia maambukizi zaidi.

Afrika kusini na Nigeria zimeripoti vifo zaidi, huku Ethiopia na Burkina Faso zikiwakaribisha madaktari kutoka China kusaidia kupambana na janga hilo.

Afrika kusini ilitangaza vifo vya watu saba kutokana na virusi vya Corona na kujumulisha idadi ya watu ambao wamekufa kutokana na virusi hivyo Afrika kusini kuwa 34.

Waziri wa afya Zweli Mkhize alisema watu 5 kati ya 7 waliokufa walikuwa na matatizo mengine ya afya yakiwemo kisukari na shinikizo la damu.

Idadi ya watu ambao wamethibitishwa kuambukizwa virusi vya Corona Afrika kusini, imeongezeka na kufikia watu 2,506.

Shughuli za kawaida zimesitishwa Afrika kusini na kutaka watu kusalia makwao kwa mda wa siku 21 zilizopita. Amri ya watu kusalia makwao itaendela kutekelezwa hadi mwishoni mwa April.

Televisheni ya China CGTV, iliripoti kwamba timu ya madaktari imetumwa Ethiopia na Burkinafaso kusaidia kupambana na maambukizi ya virusi vya Corona.

Serikali ya Nigeria inapanga kuwaalika madaktari 18 kutoka China kusaidia nchi hiyo kupambana na virusi vya Corona, japo madaktari nchini Nigeria wamesema hawakubaliana na hatua hiyo.

Muungano wa madaktari Nigeria, umesema ingekuwa vyema kwa serikali kuwaajiri madaktari wasiokuwa na ajira nchini humo badala ya kuleta madaktari wa China, wasiofahamu Maisha, utamaduni au changamoto za kufanya kazi Nigeria.

Nchini Libya, serikali inayoungwa mkono na umoja wa mataifa imetoa amri ya watu kusalia makwao siku nzima.

Amri hiyo itakayoanza kutekelezwa kesho ijumaa, itadumu kwa mda wa siku 10 katika juhudi za kukabiliana na maambukizi ya virusi vya Corona.

Libya imeripoti watu 48 wameambukizwa na COVID-19 na kifo cha mtu mmoja.

-Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA Washington DC

XS
SM
MD
LG