Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 08:56

Tanzania: Shule, vyuo kwendelea kufungwa huku maambukizi ya Corona yakiongezeka


Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa
Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa

Serikali ya Tanzania Jumanne iliagiza shule na vyuo vyote kuendelea kufungwa kwa muda usiojuliakana kama hatua mojawapo ya kudhibithi maambukizi ya virusi vya Corona.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari, waziri mkuu Kassim Majaliwa, alisema kwamba serikali pia imesitisha maadhimisho ya sherehe za mapinduzi zilizokuwa zifanyike April tarehe 26.

Sherehe za siku ya wafanyakazi (Mei 1) pia hazitafanyika.

Jumla ya watu 53 wameambukizwa virusi vya Corona nchini Tanzania kufikia wakati tunaandaa ripoti hii, idadi kubwa ikiwa katika mji wa Dar-es-salaam.

Watu wanne zaidi wamegunduliwa kuambukizwa virusi vya COVID-19 hii leo, jijini Dar-es-salaam.

Shughuli za michezo pia zitaendelea kusimama.

Taarifa hiyo inasema kwamba “Rais Dkt. Magufuli ameagiza Shilingi milioni 500 ambazo zilitengwa kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 56 ya Sherehe za Muungano zipelekwe kwenye mfuko wa kupambana na COVID-19 wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar”, na kuongezea kwamba serikali imeomba msaada wa kifedha kutoka kwa wahisani kusaidia kupamba na Corona.

“Elimu ya tahadhari ni muhimu ikaendelea kutolewa kwa wananchi ili waweze kujikinga na maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona. Kama si lazima kutoka, wananchi waendelee kutulia majumbani mwao.” Amesema Kassim Majaliwa.

Wakati huo huo, benki ya dunia imefutilia mbali taarifa inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii, inaodai kwamba Tanzania imechukua hatua nzuri zaidi na za kipekee kukabiliana na maambukizi ya virusi vya Corona, ikidai kwamba nchi zingine za Afrika zinatumia mbinu zinazotumika na mataifa ya magharibi.

Kulingana na taarifa ya Benki ya Dunia, ripoti yake ya Alhamisi April 9, kuhusu athari ya maambukizi ya virusi vya Corona katika nchi za Afrika, haitaji Tanzania mahali popote, wala kuangazia juhudi zinazochukuliwa na nchi hiyo kukabiliana na maambukizi ya virusi hivyo.

Baadhi ya wataalam wamekosoa ushauri unaotolewa na viongozi Tanzania, ukiwemo kuwataka watu kukusanyika makanisani kwa maombi kama njia ya kushinda nguvu virusi vya Corona.

Ripoti iliyochapiswa kwenye wavuti wa benki ya dunia, inasema kwamba kiwango cha ukuaji wa uchumi Afrika, kinatarajiwa kushuka kutoka 2.4% hadi -5.1%, ikiwa ndio hali mbaya zaidi ya uchumi kwa mda wa miaka 25, kutokana na janga la maambukizi ya virusi vya Corona.

Ripoti hiyo vile vile inasema kwamba itagharimu kati ya dola milioni 37 na 79 kwa uchumi kurejea hali yake ya kawaida baada ya janga la Corona.

Angola, Nigeria na Afrika kusini zenye uchumi mkubwa zaidi Afrika, zinatabiriwa kuathirika zaidi kiuchumi.

Ripoti ya benki ya dunia vile vile inaonya kwamba sekta ya utalii ndio itaathirika zaidi katika jumuiya ya Afrika mashariki.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG