Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Novemba 23, 2024 Local time: 08:45

Mstaafu wa jeshi Uingereza, miaka 99, achangisha dola milioni 15 kusaidia kudhibiti janga la corona


Mwanajeshi mstaafu Tom Moore (kulia) akiwa katika bustani yake Uingereza.
Mwanajeshi mstaafu Tom Moore (kulia) akiwa katika bustani yake Uingereza.

Janga la virusi vya corona limeleta ubunifu kwa watu wengi duniani ambao nchi zao zimetoa amri ya kutotoka majumbani, na vilevile wanaendelea kutoa misaada kwa wafanyakazi wa afya ambao wanawatibu wale waliopata maambukizi ya COVID-19.

Nchini Uingereza Alhamisi, shujaa mmoja wa vita alitekeleza azma yake ya kutembea katika bustani yake nyuma ya nyumba yake yenye ukubwa wa mita 25 kuadhimisha kutimiza kwake miaka 100 akihamasisha watu kuchangia kuboresha huduma za afya ya taifa ya nchi hiyo.

Kampeni hiyo ya kuchangisha fedha iliyoendeshwa mtandaoni mwanzoni ilikuwa imekusudia kukusanya takriban dola za Marekani 624,000. Baada ya Tom Moore kumaliza matembezi yake aliyokusudia, kampeni hiyo ilitangazwa katika televisheni mubashara, na juhudi hiyo ilikuwa imekusanya zaidi ya dola milioni 15.

Mwanajeshi huyo mstaafu amesema alikuwa ameingiwa na hamasa ya kukusanya fedha kutokana huduma aliyopokea wakati alipofanyiwa matibabu ya mfupa wa paja uliokuwa umevunjika na kutibiwa saratani.

“Nyote mnapaswa kukumbuka kuwa tutavuka katika hili mwishoni, kila kitu kitakuwa sawa, inaweza kuchukuwa muda,” Moore alisema. “Mwisho wa siku sote tutavuka salama.”

Wakati gani na vipi watu watahitimisha amri ya kutotoka nje, na vilevile kurejea kwa shughuli za biashara duniani, ni suala zito linalozikabili serikali mbalimbali.

Viongozi wameeleza nia yao ya kurudisha shughuli za uchumi, na wakishirikiana na wataalam wa afya wametahadharisha kuwa kuna haja ya kutoharakisha kuruhusu shughuli hizo za kiuchumi na hilo ni hatarishi kwa kueneza maambukizi mapya katika maeneo ambayo tayari wameanza kudhibiti kuenea kwa virusi hivyo.

Chansela wa Ujerumani Angela Merkel inampango wa kuruhusu baadhi ya shule kufunguliwa Mei 4, kufuatia mpango kama huo uliopo katika nchi nyingine za Ulaya. Amesema baadhi ya maduka yanaweza kufunguliwa wiki ijayo.

Nchini Canada, Waziri Mkuu Justin Trudeau amesema nchi yake bado haiko tayari kulegeza masharti ya kutotoka nje. Amewataka wananchi wa Canada kusubiri, akisema bado “wana wiki kadhaa mbele yao.”

Rais wa Marekani Donald Trump ni kati ya wale ambao wamekuwa wakipaza sauti zaidi akitaka shughuli za kiuchumi Marekani zianze kama kawaida ambalo ni uchumi mkubwa zaidi duniani.

Trump anatarajiwa kutangaza Alhamisi muongozo mpya, japokuwa maafisa wa afya wamesema kulegeza masharti mapema mwezi Mei itakuwa ni haraka sana, na hatimaye masharti hayo ni uamuzi wa kila gavana katika jimbo lake.

Trump pia atashiriki Alhamisi katika mkutano kwa njia ya video na viongozi wengine wa G-7 kujadili hatua zitakazo ratibiwa kwa pamoja kupambana na janga la virusi vya corona.

Rais alikosolewa upya Jumatano na Rais wa zamani wa Marekani Jimmy Carter na bilionea Bill Gates juu ya uamuzi wake wa kusitisha ufadhili kwa Shirika la Afya Duniani (WHO).

Carter ametoa tamko akisema WHO “ni shirika pekee la kimataifa lenye uwezo wa kuongoza juhudi za kudhibiti virusi hivi.”

Gates, ambaye pia ni mfadhili mkuu wa WHO, amesema uamuzi huo wa Trump “ni hatari kama unavyosikika.”

Marekani ni mfadhili mkubwa kuliko nchi zote kwa WHO, ikichangia zaidi ya dola milioni 400 mwaka 2019 ambayo ni asilimia 15 ya bajeti nzima ya taasisi hiyo.

Trump ameituhumu WHO yenye makao yake Geneva kwa kushindwa kupata taarifa zenye kujitegemea juu ya virusi vya corona vilivyoibuka kutoka mji wa kati wa Wuhan nchini China, na badala yake kutegemea ripoti rasmi ya serikali ya China.

Maafisa wa Beijing awali walijaribu kuficha hatari za virusi vipya vya corona. Trump amesema ufadhili huo utasitishwa mpaka uchunguzi ufanyike jinsi WHO ilivyoshughulikia suala hilo la mlipuko huo China.

Hivi sasa Marekani ni nchi iliyoathirika zaidi ikiwa na zaidi ya maambukizi 640,000 ya COVID-19 hadi siku ya Alhamisi, kati ya maambukizi zaidi ya milioni 2 duniani kote.

XS
SM
MD
LG