Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Novemba 05, 2024 Local time: 17:46

Wataalam wa uchumi wahoji mkopo wa China kwa Tanzania wenye thamani ya dola milioni 56.7


Rais Samia Suluhu Hassan akifanya mazungumzo na Rais wa China Xi JInping, Beijing, China. Picha kwa hisani ya Ikulu ya Dar es Salaam.
Rais Samia Suluhu Hassan akifanya mazungumzo na Rais wa China Xi JInping, Beijing, China. Picha kwa hisani ya Ikulu ya Dar es Salaam.

Hofu na wasiwasi umeibuka nchini Tanzania baada ya wataalamu wa uchumi kuhoji mkopo uliopewa Serikali wenye thamani ya dola za kimarekani million 56.7 (Tsh 129.7 Tril.) kutoka katika taifa la China.

Hoja hiyo inajiri pamoja na kuwa Tanzania imesamehewa sehemu ya deni lenye thamani ya Tsh bilioni 31.4 wakisema uchumi utadumaa na kuelemewa kwa kiasi kikubwa.

Pia wanadai kuwa hofu hiyo inatokana na serikali hiyo kutoweka mikakati madhubuti ya kupambana na ubadhirifu wa fedha za umma.

Haya yameelezwa siku chache baada ya Serikali ya Tanzania kupata mkopo na kusamehewa deni lake na serikali ya China kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa uwanja wa Ndege wa Zanzibar Terminal 3, wakati watu wengi wakidhani ni neema wabobezi wa diplomasia ya uchumi wanayatazama mambo kwa sura tofauti, wakidai kuwa Mikopo hiyo inaweza isiinufaishe nchi kama inavyotarajiwa.

Dkt Bravious Kahyoza mchumi na mhadhiri wa Chuo kikuu cha Kimataifa cha Kampala tawi la Dar es Salaam amesema mfumo wa serikali ya Tanzania ndiyo unaifanya nchi iendelee kukopa.

Pia mchumi huyo anahisi hali hii inalisukuma taifa kujiingiza katika shimo dhidi ya mapambano ya kujikwamua kiuchumi.

Rais Samia Suluhu Hassan akikaribishwa na mwenyeji wake Rais wa China Xi JInping. Picha kwa hisani ya Ikulu ya Dar es Salaam.
Rais Samia Suluhu Hassan akikaribishwa na mwenyeji wake Rais wa China Xi JInping. Picha kwa hisani ya Ikulu ya Dar es Salaam.

Kukopa na kusamehewa madeni si jambo linaloweza kuchukiza kwa jicho la kawaida lakini wasiwasi uliopo fedha hizo zinahitaji uongozi imara na thabiti katika kudhibiti mianya ya ubadhirifu wa fedha za umma, kufikia lengo husika na wananchi waweze kuona matunda yake.

Mhadhiri Mwandamizi Mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Professa Xavery Lwaitama akizungumza na Sauti ya Amerika amesema tabia ya serikali kukopa katika mazingira ambayo hakuna sera imara za kulinda mali za umma matunda ya uchumi hayatatarajiwa na badala yake anaona wananchi watabeba mzigo mkubwa zaidi.

Kwa Upande wake mchumi na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Profesa Abel Kiyondo amesema mkopo ni vyanzo vizuri vya mapato kama mikopo husika itatumika katika kuweka vitega uchumi ambavyo vitachochea maendeleo ya nchi ikiwemo miundombinu iliyokuwa bora.

Uhusiano wa China na Tanzania ni uhusiano wa muda mrefu sana wa kirafiki pamoja na kibiashara na kiuchumi. Tanzania pia inajulikana kuwa ina soko kubwa kwa bidhaa za China, huku baadhi ya watu wakihisi kuwa sasa China itaimarisha soko lake.

Imetayarishwa na mwandishi wetu Amri Ramadhani, Tanzania

XS
SM
MD
LG