Wachambuzi hao wanasema kuundwa kwa kikosi hicho ilikuwa ni upenyo ambao Rais ameutumia ili kuweza kurejesha shughuli za kisiasa bila kuathiri dhana ya uwajibikaji wa pamoja huku viongozi wa dini wakiwa na maoni tofauti.
Jumla ya mapendekezo 18 ya kikosi kazi yamewasilisha huku kubwa katika mapendekezo hayo ni kuondolewa kwa mgombea atakayejihusisha na rushwa kwenye uchaguzi na kuzuiwa kugombea uchaguzi ndani kwa miaka 10 tangu mgombea alipopatikana na hatia, kusimamishwa au kufukuzwa uanachama.
Pamoja na matokeo ya urais kuhojiwa mahakamani, matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika Tume ya Uchaguzi na rushwa katika chaguzi za ndani ya vyama na uchaguzi mkuu.
Mapendekezo hayo ni baada ya Rais Samia kuunda kikosi kazi suala ambalo mchambuzi wa kisiasa na kijamii kutoka chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) Dkt. Paul Loisulie, amesema isingekuwa busara Rais kuingia madarakani na kutoa amri ya shughuli za kisiasa kurejea bila ya kupitia mchakato wowote huku akisema ripoti hiyo itafungua ukurasa mpya kwa siasa za Tanzania.
Aidha Askofu Emmaus Mwamakula Mkuu wa Kanisa la Moravian la Uamsho Tanzania akizungumza na Sauti ya Amerika amesema waliositisha mikutano ya hadhara wamevunja katiba ya Tanzania hivyo wanapaswa kuchukuliwa hatua na siyo kupongezwa huku wale wanaodai katiba wakichukuliwa kuwa ni magaidi.
Naye Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Alhad Mussa Salum ametoa wito kwa viongozi wa kisiasa na wananchi kuwa wavumilivu kwa kuwa kuna kazi kubwa ambayo imefanyika na kuachana na tabia ya kupinga kila kitu.
Hata hivyo kikosi kazi hicho kikiwa kimemaliza kazi yake Rais Samia aliongezea kusema mapendekezo yao si amri kwa Serikali suala ambalo limeibua hisia tofauti kwa wanasiasa hasa wa upinzani.
Imeandaliwa na Amri Ramadhani Sauti ya Amerika Dar es Salaam