Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 00:58

UNICEF yalaani shambulizi lililouwa watu 16 wasiokuwa na hatia DRC


Waathirika wa mauaji huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wakiwa katika kambi ya muda baada ya kulazimika kukimbia makazi yao kutokana na mauaji huko Bunia, jimbo la Ituri, Juni 25, 2019.
Waathirika wa mauaji huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wakiwa katika kambi ya muda baada ya kulazimika kukimbia makazi yao kutokana na mauaji huko Bunia, jimbo la Ituri, Juni 25, 2019.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF, limelaani vikali shambulizi ambalo limeua watu 16, wakiwemo wasichana watano walio na umri wa chini ya miaka 15, Juni 3 katika jimbo la Ituri mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).

Mwakilishi wa UNICEF huko DRC, Edouard Beigbeder, amesema “tunalaani vikali sana shambulizi hilo kwa watoto wasiokuwa na hatia.” amezitaka pande zote kuheshimu haki za wanawake na watoto.

Kwa mujibu wa ripoti ambazo zimethibitishwa na Umoja wa Mataifa (UN) shambulizi limefanyika katika eneo la Moussa, katika kijiji kimoja kwenye eneo la Djugu, kaskazini mwa mji mkuu wa jimbo, Bunia. Waathirika 16 ambao waliwahi kuwa watu wasiokuwa na makazi walirejea kijijini hapo na kuuawa katika shambulizi la bunduki na visu. Matokeo yake, dazeni ya watu wamekimbia kutoka Moussa na kuchukua hifadhi katika vijiji jirani.

Zaidi ya watu 300 wamefariki hadi hivi sasa ikiwa ni matokeo ya ghasia zinazoendelea katika jimbo la Ituri tangu mwanzoni mwa mwaka 2020. Mwezi Aprili na Mei pekee, UNICEF imepokea zaidi ya shutuma 100 za ukiukaji mkubwa sana wa haki za watoto, kama vile ubakaji, mauaji na ukataji wa viungo, na mashambulizi kwenye shule na vituo vya afya huko Ituri.

Mwezi uliopita UNICEF ilionya kwamba hali ya usalama huko Ituri inazidi kudorora kwa kasi na kuitaka jumuiya ya kimataifa na serikali ya DRC kuchukua hatua za haraka kuepusha mzozo ambao utawalazimisha watoto wengi zaidi kuondoka katika eneo na kuhatarisha maisha yao.

Zaidi ya watu 200,000, wengi wao watoto, wamekimbia ghasia mbaya za maeneo ya Djugu, Mahagi na Irumu katika jimbo la Ituri tangu mwanzoni mwa mwaka huu. Wengi wao wamepewa hifadhi na jamii wenyeji na kwenye makazi yenye msongamano mkubwa sana katika vituo vya watu wasiokuwa na makazi ndani na kuzunguka Bunia.

Imetayarishwa na mwandishi wetu, Khadija Riyami, Washington, DC

XS
SM
MD
LG