Shirika la Habari la Reuters Jumamosi lilinukuu duru zilizoarifu kwamba watu wasiopungua 16 wamepoteza maisha yao kwenye shambulizi hilo, huku shirika la Habari la Ufaransa AFP, likikadiria idadi ya waliokufa kuwa takriban 13, kwa mujibu wa mkurugenzi wa taasisi ya kuhifadhi mazingira ya Kongo, Cosma Wilungula.
Taarifa iliyotolewa na maafisa wa serikali imeeleza kwamba "shambulizi kubwa" lililotekelezwa na watu wanaodhaniwa kuwa wanamgambo, lilisababisha maafa makubwa katika Kijiji cha Rumangabo.
Kati ya waliouawa ni wanakijiji na maafisa wa kulinda misitu na wanyamapori.
Hata hivyo, hadi tulipokuwa tukitayarisha ripoti hii, hakuna mtu au watu waliokuwa wamedai kutekeleza shambulizi hilo.
Mbuga ya Virunga, imekuwa kitovu cha mashambulizi ya mara kwa mara yanayotekelezwa na wanamgambo mbalimbali, wakiwemo wale wa FDLR, wanaodai kwamba ni wakombozi wa Rwanda.