Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 22:50

Wasaidizi waTshisekedi wahofiwa kufariki katika ajali ya ndege DRC


Rais Tshisekedi akiwa katika ziara Goma.
Rais Tshisekedi akiwa katika ziara Goma.

Watu 27 waliokuwa ndani ya ndege iliyokuwa ikisafirisha wasaidizi na vifaa vya msafara wa Rais Tshisekedi katika mji wa Goma, Alhamisi, wanahofiwa kupoteza maisha, radio ya Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imeripoti Ijumaa.

Ndege hiyo ya kubeba mizigo aina Antonov 72 ilipotea angani baada ya kuruka kutoka mjini Goma kuelekea katika mji mkuu Kinshasa. Mamlaka ya usafiri wa anga imethibitisha kwamba ndege hiyo ilipoteza mawasiliano na kituo cha usafiri wa anga kuanzia saa tisa mchana majira ya DRC. Mamlaka hiyo inasema watu 8 waliokuwa ndani ya ndege hiyo wamefariki.

Radio OKAPI ya Umoja wa Mataifa ikinukuu vyanzo vya ikulu ya DRC imesema watu 27, wakiwemo walinzi wa Rais Tshisekedi, dereva wake na wasaidizi wake ndio waliokuwa ndani ya ndege hiyo, na wote wanahofiwa wamefariki.

Taarifa zimeendelea kusema kwamba mabaki ya ndege hiyo iliyoanguka yaliokotwa katika jimbo la Maniema.

Hayo yakiarifiwa, wafuasi wa chama cha UDPS cha Rais Felix Thisekedi wameandamana Ijumaa asubuhi katika barabara za mji mkuu Kinshasa, ili kuonyesha hasira zao kutokana na kupotea kwa ndege hiyo. Waandamanaji hao ambao wamechoma matairi na kuweka vizuizi barabarani, wanaomba uchunguzi ufanyike ili kujuwa kilichosababisha ajali ya ndege hiyo.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu Patrick Nduwimana, Washington, DC.

XS
SM
MD
LG