Rais Volodymyr Zelenskyy alisema katika hotuba yake ya kila siku ya Jumamosi, “Nakumbuka kile ‘washauri’ mbalimbali walichonieleza na kunishauri wakati ule. … Najua wengi wao hivi sasa wanaona aibu kwa kwa maneno waliyosema wakati huo. … Wananchi wa Ukraine wathibitisha kuwa watu wetu wana nguvu hawawezi kushindwa, walinzi wetu wana nguvu hawawezi kushindwa.”
Zelenskyy alisema, “Sisi bado tunahitaji kupigana, bado tunahitaji kufanya mambo mengi, bado tunahitaji kuvumilia na kustahamili, bahati mbaya, kuna machungu mengi. … Lakini wananchi wa Ukraine wana haki ya kujivunia wenyewe, nchi yao, na mashujaa wao.
“Ni lazima tutambue,” aliongeza “kuwa wiki hii Russia inaweza kutaka kujaribu kufanya kitu kiovu hasa, kitu hasa cha ukatili. Hivyo ndivyo alivyo adui yetu. Lakini katika wiki nyingine yoyote wakati wa miezi hii sita, Russia ilifanya jambo hilo hilo kila wakati – lililo ovyo na la ukatili.
Jeshi la anga la Russia iliitungua ndege isiyo na rubani drone huko Crimea Jumomosi, mamlaka za Russia zilisema. Lilikuwa ni tukio la pili kama hilo katika makao makuu ya Manowari zilizoko Bahari ya Black Sea katika wiki tatu.
Oleg Kryuchkov, msaidizi wa gavana wa Crimea, pia alisema bila ya kufafanua kuwa “mashambulizi ya ndege ndogo ndogo zisizo na rubani” yalikabiliwa na ulinzi wa anga huko Crimea magharibi.
Russia inaiona Crimea ni eneo lake, lakini maafisa wa Ukraine hawajawahi kukubali uvamizi huo wa mwaka 2014.
Mikhail Razvozhaev, gavana wa Sevastopol, alisema kuwa droni hiyo ilitunguliwa na kuangukia kwenye paa la makao makuu ya manowari za Russia lakini haikusababisha vifo au uharibifu mkubwa.
Razvozhaev aliposti taarifa mpya kwa njia ya mawasiliano ya Telegram Jumamosi usiku akiwataka wakazi kuacha kuchukua video na kusambaza picha za mfumo wa ulinzi wa kutungua ndege wa eneo hilo na kuonyesha jinsi unavyofanya kazi, shirika la habari la Reuters limeripoti.
Tukio hilo linaeleza namna majeshi ya Russia yalivyokuwa hatarini huko Crimea.