Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Novemba 23, 2024 Local time: 10:16

Ufaransa: Viongozi na wataalam wakutana kujadili kupunguza mzigo wa madeni kwa nchi zenye kipato cha chini


Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akifungua mkutano wa viongozi na wataalam mjini Paris, Ufaransa.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akifungua mkutano wa viongozi na wataalam mjini Paris, Ufaransa.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amefungua mkutano wa viongozi na wataalam mjini Paris Alhamisi juu ya hali ya hewa, wenye lengo la kutayarisha mpango wa kupunguza mzigo wa madeni  kwa mataifa yenye kipato ya chini.

Mkutano huo pia utajadili suala la kutolewa fedha zaidi kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa pamoja na kuanza mpango wa mfumo mpya wa fedha duniani.

Mkutano huo wa ngazi ya juu wa siku mbili unawaleta pamoja karibu viongozi 50 katika mji mkuu wa Ufaransa, Paris ili kujaribu kufikia maridhiano juu ya namna ya kuendelea mbele na baadhi ya mipango ya kimataifa ambayo inasuasua inayosimamiwa na mashirika makuu kama Umoja wa Mataifa, Benki Kuu ya Dunia na G20.

Akiufungua mkutano huo Rais Macron amewaambia viongozi wenzake kwamba hakuna nchi iliyokuwa na hiari ya kuchagua kati ya kukabiliana na umaskini na kushughulikia mabadiliko ya hali ya hewa.

Emmanuel Macron, Rais wa Ufaransa: Hali ya ukosefu wa usawa inaongezeka, athari za hali ya hewa zinazidi kusababisha hatari, na dunia yetu inazidi kukabiliwa na matatizo makubwa. Janga limeweza kumulika changamoto hizi zote na hivi sasa vita nchini Ukraine kufuatia uvamizi wa Russia na migogoro chungu nzima. Tuna mfumo wa fedha uliofanya kazi vyema uliokuwa na manufaa makubwa wakati ya miongo iliyopita, lakini hivi sasa haufai tena, ni mfumo usioambatana na hali halisi ilivyo na hivyo tunahitaji kufanya marekebisho.

Serikali ya Ufaransa imeitisha mkutano huo ili kutayarisha mipango ya kuwezesha majadiliano kuwa rahisi zaidi kabla ya mikutano muhimu ya kiuchumi na fedha inayotarajiwa kufanyika katika siku na miezi inayokuja, kama mkutano wa Bricks na ule wa kundi la mataifa 20 tajiri G20.

Akizungumza baada ya Rais Macron mwanaharakati wa mabadiliko ya hali ya hewa kutoka Uganda Vanessa Nakate aliwataka viongozi wanaohudhuria kukaa kimya kwa dakika moja ili kutoa heshima kwa watu wanaotaabika kutokana na majanga duniani.

Vanessa Nakate Mwanaharakati wa mabadiliko ya Hali ya hewa: Inabidi tuwalazimishe wachafuzi mazingira kulipa. Ni lazima kufuta madeni na kupata mipango mizuri zaidi kugharimia athari za mabadiliko ya hali ya hewa katika nchi za kusini mwa dunia ili zisilazimike kugharimia janga hili ambalo hawajalisababisha. Ni lazima mfikiriye juu ya matrilioni na wala si mabilioni .

Waziri mkuu wa Barbados Mia Mottley anaewakilisha mataifa yanayoendelea kwenye mkutano huo anawasilisha mapendekezo ya mataifa yanayofahamika kama mipango ya Bridgetown.

Mia Amor Mottley
Mia Amor Mottley

Mia Mottley, waziri mkuu wa Barbados anaeleza: "Na tunazungumzia mageuzi kamili kuweza kupata mitaji, hata kama ni jambo lisilopendwa na wengine. Sisi hatuombi kufilisi mashirika ya kibinasi. Hayo sio maombi yetu. Lakini tunamuomba kila mtu abebe mzigo wa matatizo ili tuweze kufurahia sote neema inayopatikana. Hii ina maana wakati umefika kuyaleta kwenye meza ya mazungumzo mashirika makuu ya kimataifa ambayo faida zao ni karibu theluthi mbili ya mapato ya mataifa yote ya dunia.

Barbados imewasilisha pia mpango kamili wa jinsi ya kurekebisha mfumo wa fedha duniani kusaidia nchi zinazoendelea kuwekeza katika nishati mbadala safi na kuimarisha mipango ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa.

Miongoni mwa viongozi wanaohudhuria mkutano huo ni viongozi kutoka mataifa 10 ya Afrika, katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, Mkurugenzi wa Shrika la fedha la kimataifa IMF Kristalina Georgieva, Rais wa Benki ya Dunia, Ajay Banga na Waziri wa Fedha wa Marekani Janet yellen.

Nje ya mkutano huo katika sehemu mbali mbali za Paris wanaharakati wa mabadiliko ya hali ya hewa wamekuwa wakiandamana na kukusanyika na kutoa wito wa kusitisha matumizi ya mafuta ghafi na kutekelezwa makubaliano ya mabadiliko ya hali ya hewa.

Chanzo cha habari hii ni mashirika ya habari ya AFP na Reuters.

Forum

XS
SM
MD
LG