Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 24, 2024 Local time: 08:04

Uchumi wa Kenya washuka kwa asilimia 0.3 kutokana na COVID-19


Rais Uhuru Kenyatta
Rais Uhuru Kenyatta

Ukuaji wa uchumi Kenya umeshuka kwa kiwango cha asilimia 0.3 mwaka 2020 kutokana na athari za janga la virusi vya corona, licha ya uchumi huko kukua kwa asilimia 5 mwaka 2019.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotangazwa Alhamisi na Waziri wa Fedha, Ukur Yattani, kiwango cha mfumuko wa bei kilipanda kutoka asilimia 5.3 mwaka 2019 hadi asilimia 5.4 mwaka 2020 kutokana na mikakati ya kudhibiti maambukizi ya virusi vya Corona, iliyodumaza usambazaji wa bidhaa.

Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2021 zinazoangazia mwaka 2020 kuhusu maendeleo ya uchumi Kenya, pato la taifa kutoka sekta ya utalii limepungua kwa asilimia 43.9 hadi shilingi bilioni 91.7 mwaka 2020 huku idadi ya wageni kwenye mahoteli ilipungua kwa asilimia 58.0 mwaka huo hadi watu milioni 3.8.

Idadi ya wageni waliowasili Kenya mwaka 2020 ilipungua kwa asilimia 71.5 hadi 579,600 ikilinganishwa na mwaka 2019.

Kiwango cha biashara kilipungua hadi shilingi trilioni 2.29 huku thamani ya bidhaa zilizoingizwa Kenya ikiwa ni shilingi trilioni 1.64 wakati thamani ya bidhaa zilizosafirishwa nje ya nchi ikiwa ni shilingi trilioni 0.64.

Abiria wakiwa wamevaa vifaa vya kujikinga na COVID-19 wakishuka uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta Nairobi, Kenya, on January 19, 2021.
Abiria wakiwa wamevaa vifaa vya kujikinga na COVID-19 wakishuka uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta Nairobi, Kenya, on January 19, 2021.

Kwa usafiri wa ndege, idadi ya wasafiri ilipungua kwa asilimia 62.5 kutoka watu milioni 12.0 waliosafiri Kenya mwaka 2019 hadi watu milioni 4.5 mwaka 2020 wakati kiwango cha mizigo kikipungua kwa asilimia 8.9

Kiwango cha mfumuko wa bei za bidhaa kilipanda kutoka asilimia 5.3 mwaka 2019 hadi asilimia 5.4 mwaka 2020 kutokana na mikakati ya serikali ya kudhibiti maambukizi ya virusi vya Corona, iliyolemaza usambazaji wa bidhaa na kuongeza bei za bidhaa hasa katika sekta ya uchukuzi na nishati, serikali inatarajia kiwango hicho kitaongezeka hadi mwishoni mwa mwaka 2021.

Lakini wakati pato la mataifa yalio kusini mwa jangwa la Sahara likipungua kwa asilimia 1.9 mwaka 2020 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 3.2 mwaka 2019, serikali ya Kenya inaeleza kuwa sekta ya kilimo ilinawiri kwa asilimia 4.8 kutokana na uzalishaji na uuzaji wa kiasi cha juu wa chai, maharage, mchele na mtama na kiwango cha juu cha mvua kilichoshuhudiwa mwaka huo.

Charles Karisa, mshauri wa masuala ya uchumi nchini Kenya anaeleza kuwa Kenya haikuwekeza kwenye sekta muhimu kukinga uchumi wake.

“Lakini je, ni kwa kiasi gani Kenya inaweza kujikwamua licha ya athari iliyosababishwa na virusi vya Corona?” Karisa anaeleza tena.”

Aidha, Yattani, anaeleza kuwa sekta ya habari, mawasiliano na teknolojia ilinawiri kwa asilimia 4.8 kutokana na ongezeko la matumizi ya mifumo ya kiteknolojia ya kupokea na kutuma pesa kutumia simu na matumizi ya mifumo hiyo katika mafunzo wakati vituo vya mafunzo viliathirika kutokana na maambukizi ya virusi vya Corona.

Waziri Yattani, ameeleza kuwa ajira katika sekta mbalimbali za uchumi ziliathiriwa vibaya na hatua za kuzuia kuenea kwa virusi vya Corona lakini kwamba nyingi ya asilimia 83 ya ajira zilizopatikana mwaka 2020, zilitoka kwenye sekta ya biashara ndogo ndogo.

Hata hivyo, serikali ya Kenya ina matumaini kuwa kutokana na mikakati mbalimbali iliyoweka, uchumi wake mwishoni mwa 2021 utanawiri baada ya kupondwapondwa na virusi vya Corona.

“Kutokana na yale ambayo tumeyaona, tuna imani na matumaini mengi kuwa uchumi wetu utakua kwa zaidi ya asilimia 6, hii kuashiria kuwa tutakuwa na nafasi nyingi za ajira na kuinuka na kunawiri kwa sekta mbalimbali za kiuchumi kukidhi matatizo yetu,” amefafanua Waziri Yattani.

Mwandishi wetu Kennedy Wandera, Nairobi, Kenya

XS
SM
MD
LG