Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 24, 2024 Local time: 15:53

Benki ya Dunia yatishia kutathmini upya ufadhili Kenya


Bango la Benki ya Dunia na Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta.
Bango la Benki ya Dunia na Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta.

Hatua ya serikali ya Kenya ya kusitisha mchakato wa ujenzi wa miundombinu katika shule za upili, katika mradi uliyofadhiliwa na Benki Kuu ya Dunia, wa shilingi bilioni 22.8, huenda ikaathiri makubaliano yaliyoafikiwa awali kati ya serikali na taasisi hiyo ya ufadhili wa kimataifa.

Katika makubaliano yaliyotiwa saini kati ya Kenya na Benki Kuu ya Dunia (WB), nchi hiyo ingepata ufadhili wa Shilingi bilioni 22.8 kati ya mwaka wa 2017 na 2023, ili kuimarisha miundombinu katika shule za sekondari, na kuziwezesha kuwapa nafasi wanafunzi wote waliomaliza masomo ya shule za msingi.

Mpango huo pia ulikusudiwa kuiwezesha serikali kuwaajiri walimu wa ziada, kutoa mafunzo kwao, na pia kufadhili masomo kwa wanafunzi wanaotoka kwa familia maskini, pamoja na kugharamia mabadiliko ya mtaala wa elimu.

Kwa jumla, shule zipatazo 110 katika kaunti 30 zingefaidika.

Lakini sasa, mpango huo umeingia tashwishi baada ya Rais Uhuru Kenyatta kumuagiza Waziri wa elimu George Magoha, kutathmini upya mahitaji katika sekta ya elimu, hatua ambayo, benki ya dunia inasema, ni mchakato unaochukua muda mrefu kuliko ilivyotarajiwa, na kuonya kwamba huenda ikalazimika kufanya upya makubaliano ya ufadhili huo.

Wachambuzi wanasema hatua hiyo huenda ikawa na gharama kubwa kwa Kenya katika siku za usoni.

Gazeti la Daily Nation la Kenya, limeripoti kwamba limepata nyaraka za faragha zilizotumwa kwa waziri wa elimu, kumtaka asitishe utoaji wa fedha kwa mradi huo.

Haya yanajiri huku viwango vya elimu vikitajwa na wachambuzi kama vilivodorora kwa sababu ya miundombinu dhaifu.

Jackline Adhiambo, mchambuzi wa masuala ya elimu nchini Kenya, anasema serikali haijatoa sababu za kuaminika kuhusu hatua hiyo.

“Kabla ya kuomba ufadhili huo kutoka kwa Benk Kuu ya Dunia, walikuwa wamefanya tathmini kuhusu hali ya miundombinu. Iweje sasa wanataka tena kufanya tathmnini?” Aliuliza Bi Adhiambo katika mahojiano na idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika.

Mkuu wa Utumishi wa Umma wa Kenya Joseph Kinyua alimwandikia barua Waziri wa elimu mapema mwaka huu akisema kwamba serikali ilikuwa ikiandaa majibu ya kisera kwa changamoto zinazokabili sekta ya elimu ya sekondari, na kwamba ilikuwa ni lazima kusitisha miradi yote ya maendeleo wakati wa tathmini hiyo.

Mwezi Aprili mwaka huu, mkurugenzi anayewakilisha Benki ya Dunia nchini Kenya, Keith Hansen, alionya kuwa ucheleweshaji unaweza kufanya mradi huo kukosa kufikia ratiba yake, kama ulivyopangwa kukamilika mwaka 2023 na kusababisha kuanza tena mchakato wa zabuni. Alisema Benki kuu ya dunia imeridhika na kandarasi zilizotolewa kwa makampuni 17, lakini ina wasiwasi kuhusu kasi ndogo ya mchakato wenyewe. George Ochieng, mwanaharakati wa masuala ya elimu nchini Kenya, anahisi kwamba hali hiyo huenda ikapelekea visa vya ufisadi.

“Kuchelewesha huko ndiko hupelekea pesa kuanza kupotea na viendo vya ufisadi kuongezeka. Ningeisihi serikali kuharakisha mchakato huo ili kupunguza changamoto zinazowakabili wanafunzi na walimu katika sehemu mbalimbali za nchi kwa sasa,” alisema Ochieng.

Serikali imesisitiza kwamba baada ya kuanza mchakato wa kuhakikisha kwamba kila manafunzi aliyemaliza masomo katika shule za msingi anapata nafasi katika shule za sekondari, imegundua kuwa miundombinu iliyokuwepo haiwezi kustahimili mipango hiyo mipya na kwamba huenda kukahitajika kiasi kikubwa zaidi cha fedha kugharamia hatua hizo.

XS
SM
MD
LG