Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Desemba 25, 2024 Local time: 08:48

Shirika la Chakula Duniani WFP la shinda Tuzo ya Amani ya Nobel 2020


Alain Noudehou, Mratibu wa Huduma za dharura UN South Sudan, na Matthew HollingWorth, mkurugenzi miami wa WFP, wapiti kwenye mafuriko huko Duk Padiet wilaya ya jimbo la Jonglei nchini Sudan Kusini, Sept. 24, 2020.
Alain Noudehou, Mratibu wa Huduma za dharura UN South Sudan, na Matthew HollingWorth, mkurugenzi miami wa WFP, wapiti kwenye mafuriko huko Duk Padiet wilaya ya jimbo la Jonglei nchini Sudan Kusini, Sept. 24, 2020.

Shirika la Chakula Duniani (WFP) limeelza kuridhika kwake kupata tuzo mashuhuri ya amani ya Nobel na kusema ni ushindi unaozingatia umuhimu wa kumaliza ghasia, mapigano na njaa duniani.

Kamati ya tuzo ya Nobel mjini Oslo Norway hii leo imeipatia WFP tuzo ya amani ya Nobel leo ya mwaka huu, kutokana na juhudi zake za kukabiliana na njaa pamoja na ukosefu wa chakula duniani.

Akitangaza ushindi huo mwenyekiti wa kamati ya Nobel Berit Reiss Anderson ushindi huo, amesema kuwa janga la virusi vya corona limeongeza hali ya njaa kwa mamilioni ya watu kote ulimwenguni na kuomba serikali kuhakikisha kuwa WFP pamoja na mashirika mengine ya kutoa misaada yanapata ufadhili unaohitajika ili kukabiliana na tatizo hilo.

"Haja ya Ushirikiano wa kimataifa imekuwa kubwa zaidi sasa kuliko wakati mwingine wowote ule. Kamati ya Nobel ya Norway imeamua kuipatia WFP tuzo ya mwaka 2020 kutokana na juhudi zake za kupambana na njaa duniani kwa juhudi zake za kuleta amani kwenye maeneo ya ghasia kwa kuhakikisha kuwa tatizo la njaa halitumiki kama silaha ya vita na mapigano," amesema Anderson.

Msichana wa kisomali akimbeba dadake wakisubiri kupewa chakula kutoka WFP mjini Mogadishu
Msichana wa kisomali akimbeba dadake wakisubiri kupewa chakula kutoka WFP mjini Mogadishu

Mwaka 2020 kulikuwa na orodha ya wagombea 211 na mashirika 107 yalioteuliwa kupata tuzo za Nobel kabla ya tarehe ya mwisho iliowekwa ya Februari 1.

Hata hivyo kamati ya Nobel ina utamaduni wa kuweka siri mshindi wa tuzo hiyo inayoheshimiwa sana ulimwenguni. Tuzo yenyewe huandamana na takriban dola milioni 1.1 za Kimarekani pamoja na medali ya dhahabu ambazo hukabidhiwa mshindi mjini Oslo kila Decemba tarehe 10 ikiwa siku ambayo mwanzilishi wa tuzo hizo Alfred Nobel alipofariki.

Kupitia ujumbe wa Twitter, WFP limesema kuwa ushindi huo ni ujumbe muhimu unaokumbusha ulimwengu kuwa kupambana na njaa ni njia moja ya kuhakikisha kuna amani. Kupitia msemaji wake Tomson Phiri, shirika hilo linasema kuwa ni heshima kubwa kwao kupata tuzo hiyo.

"Tunajivunia sana ushindi huu. Kuwepo kwenye orodha ya walioteuliwa kupokea tuzo hiyo tayari ilikuwa ni heshima kubwa. Nimelitumikia shirika hili kwa miaka 9 sasa na nimeshuhudia namna watu wanavyojitolea kuleta mabadiliko ulimwenguni. Kabla ya mimi kuhamia makao makuu mjini Geneva, nikuwa Sudan kusini ambako nilishuhudia watu wakitembea kwa miguu ili kufikishia wenzao misaada. Ni heshima kubwa kwangu kuwa sehemu ya timu iliopata ushindi huu," amesema Phiri

WFP ambayo ni shirika moja wapo ya mashirika ya Umoja wa Mataifa lilibuniwa 1961, na mwaka uliopita lilisaidia zaidi ya watu milioni 97 kwa kutoa resheni bilioni 15 za chakula kwenye takriban mataifa 88 kote duniani.

Waatalamu wanasema kwamba licha ya juhudi kubwa za kuangamiza baa la njaa duniani kufikia 2030, hali ilioko inaashiria huenda hilo lisiwezekane kulingana na wanavyosema wataalam.

Wameongeza kusema kuwa kwa kawaida wanawake na watoto ndiyo huathiriwa zaidi na njaa. Mapigano mengi yanasemekana kusababishwa na njaa ingawa pia yanasababisha hali hiyo.

WFP imesema kwamba watu walioko kwenye mataifa yanayoshuhudia vita wana uwezekano mkubwa zaidi wa kukumbwa na njaa wakilinganishwa na wale walioko kwenye mataifa yenye amani.

XS
SM
MD
LG