Umoja wa Mataifa umeanzisha uchunguzi kuhusiana na madai ya unyanyasaji wa kingono dhidi ya baadhi ya maafisa wao kaskazini mashariki mwa Karamoja, nchini Uganda.
Uchunguzi huo wa kamati maalum ya Umoja wa Mataifa ulioanza mapema mwezi huu unafuatia madai ya manyanyaso ya kingono na dhuluma dhidi ya mwanamke na mfanyakazi wa shirika hilo katika eneo la Karamoja.
Inadaiwa kwamba baadhi ya wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa walikuwa wakiwalazimisha wanawake kufanya nao tendo la ngono kwa kubadilishana na chakula.
Wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa pia wanadaiwa kuingiza wanawake katika kambi ya umoja huo kwa ngono ya kulipwa katika wilaya ya Moroto.
Wafanyakazi hao wanaishi kwenye kambi ya shirika la kutoa chakula duniani WFP katika sehemu ya Karamoja ambayo zaidi ya watu 500,000 wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula.
“Tumearifiwa kuhusu madai dhidi ya wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa wanaoishi katika kambi ya WFP mjini Moroto. Tunachunguza madai hayo” amesema Amanda Lawrence Brown, msemaji wa WFP akiwa Nairobi, Kenya.
Brown ameongezea kusema kwamba hakuna mfanyakazi wa Umoja wa Mataifa, au mtu yeyote anayeishi katika kambi ya WFP anaruhusiwa kujihusisha katika unyanyasaji wa kingono au wa aina yoyote ile dhidi ya watu katika sehemu wanafanya kazi zao.
Hata hivyo, amekataa kusema idadi ya wafanyakazi wanaoishi kwembe kambi ya Moroto kutokana na sababu za kiusalama.
Amesema kwamba uchunguzi pia unafanyika kuhusu ripoti za kuvunjwa kwa kanuni za kiusalama, na kwamba walinzi wanastahili kuwachunguza wageni wote wanaoingia katika kambi hiyo.
Mratibu mkuu wa shughuli za umoja wa mataifa nchini Uganda Rosa Malango, amesema kwamba alichukua hatua za kutaka uchunguzi kamili kufanyika kuhusiana na swala hilo.
“Natarajia kupata majibu kutoka kwa wakuu wa umoja wa mataifa ikiwemo kuwasimamisha kazi kwa mda maafisa waliohusika wakati uchunguzi unapoendelea,” ameandika Malango katika ujumbe wa barua pepe kwa viongozi wa juu wa umoja wa mataifa.
Malango amesisitiza kwamba Umoja wa mataifa haukubali kabisa unyanyasaji wa kingono na kwamba swala hilo linachunguzwa vipasavyo.
Inaripotiwa kwamba kundi la maafisa wa umoja wa mataifa walikosoa sana barua pepe aliyoandika Malango iliyofananisha Uganda na Haiti kutokana na madai hayo ya unyanyasaji wa kingono.
Kundi hilo limesema kwamba barua pepe ya Malago ina habari ambazo ni za siri san ana hangeituma kwa makundi ya ndani ya wafanyakazi wa umoja wa mataifa.
Kwa kusema kwamba Uganda ilikuwa inakaribia kufanana na Haiti, Malago alizingatia sakata ya shirika la Oxfarm ya kufunika ukweli kuhusu madai ya wafanyakazi wa shirika hilo la Uingereza kuwanyanyasa kingono waathiriwa wa tetemeko baya la ardhi la mwaka 2010, waliotegemea msaada wa chakula kutoka kwa shirika hilo.
Malago hata hivyo ansema kwamba barua yake kwa shirika la umoja wa mataifa, haingetumwa kwa watu ambao hawafanyi kazi katika umoja wa mataifa.
Hii ni mara ya pili Umoja wa Mataifa unajipata katika sakata inayohusisha eneo la Karamoja. Mwaka 2019, watu 4 waliugua baada ya kukula chakula kilichokuwa kimetolewa kama msaada na shirika la chakula duniani WFP na shirika hilo likashutumiwa kwa uzembe.
Eneo hilo lililo mpakani na Kenya, linakabiliwa na hali ngumu ya maisha kutokana na kiangazi cha kila mwaka.
Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC.