Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Januari 22, 2025 Local time: 21:02

Sarafu ya Kenya inaendelea kushuka dhidi ya dola ya Marekani


Mfanyakazi wa kiwanda cha kuhifadhia mimea huko Naivasha akisukuma mkokoteni uliojaa maua ya waridi yaliyokuwa yakisafirishwa kwa ajili ya kuuzwa nje katika soko la Ulaya. Picha na REUTERS/Thomas Mukoya.
Mfanyakazi wa kiwanda cha kuhifadhia mimea huko Naivasha akisukuma mkokoteni uliojaa maua ya waridi yaliyokuwa yakisafirishwa kwa ajili ya kuuzwa nje katika soko la Ulaya. Picha na REUTERS/Thomas Mukoya.

Kushuka kwa thamani ya sarafu ya Kenya kunamaanisha kuwa Wakenya wanatakiwa kufanya kazi zaidi na kuongeza kiwango na ubora wa uzalishaji katika soko la kimataifa.

Sarufi ya Kenya, taifa lenye uchumi mkubwa Afrika Mashariki, imekuwa ikishuka kufikia kiwango cha chini sana cha shilingi 150 kwa dola Jumatatu wiki hii, na kuongeza masaibu kwa Wakenya ambao tayari wameathiriwa na kupanda kwa gharama ya maisha.

Shilingi ya Kenya imekuwa ikishuka na kuvunja rekodi, na kusababisha upungufu wa fedha za kigeni na hivyo kuongeza changamoto katika uingizaji wa bidhaa nchini humo ikiwemo mafuta.

Wakizungumza na Sauti ya Amerika, wachumi wamesema, kwa nchi kama Kenya ambayo inajua kuidhibiti sarafu yake, kupungua thamani kwa sarafu hiyo kutasababisha ongezeko katika manunuzi ya bidhaa za Kenya zinazouzwa nje ya nchi iwapo uzalishaji utaongezeka.

Wakulima wakipanda magugu ya mwani ambayo husafirishwa na kuuzwa nje ya nchi. Picha na REUTERS/Joseph Okanga
Wakulima wakipanda magugu ya mwani ambayo husafirishwa na kuuzwa nje ya nchi. Picha na REUTERS/Joseph Okanga

Profesa Tabitha Wagith Kiriti-Nganga katika kitengo cha Uchumi, Maendeleo na Idadi ya watu katika Chuo Kikuu cha Nairobi aliiambia Sauti ya Amerika, kushuka kwa shilingi ya Kenya kutawafanya raia wafanye kazi kupita kiasi ili kufidia kupanda kwa bei za bidhaa zinazouzwa nje ya nchi.

Amesema “bidhaa zinazouzwa nje ya nchi zinauzwa kwa bei ya chini kulingana na bajeti ya fedha zinazohitajika katika uingizaji wa bidhaa ndani ya nchi” kwa hiyo “kiwango kikubwa cha shilingi kinatumika kununua dola”

Meneja wa zamani wa Benki ya Dunia anayeshugulikia mahusiano ya nje kwa nchi za Afrika na pia mkuu wa zamani wa kitengo cha mahusiano na mawasiliano katika Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) Eric Chinje amesema rais William Ruto pamoja na benki kuu wanaelewa fika athari za kushuka kwa sarafu hiyo na inawezekana ikawa mkakati katika kuongeza mauzo ya bidhaa za Kenya katika soko la dunia.

Amesema iwapo wakenya watazalisha kiwango kikubwa cha bidhaa hizo, wataweza kuipa nguvu sarafu ya nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Sarafu ya Kenya imekuwa ikishuka kwa miaka kadhaa na kuporomoka kwa takriban asilimia 24 mwaka jana, kutokana na shinikizo la viwango vya juu vya deni na kupungua kwa mapato ya serikali.

“Benki kuu inataka sarafu ya Kenya kutafuta thamani yake ya kweli katika soko la dunia” alisema na kuongeza kuwa uzalishaji na usafirishaji wa bidhaa hizo katika soko la kimataifa kutaleta uwiano na kubadili mkondo wa shilingi hiyo.

Wafanyikazi katika kiwanda cha nguo huko Nairobi. Picha na REUTERS/Baz Ratner
Wafanyikazi katika kiwanda cha nguo huko Nairobi. Picha na REUTERS/Baz Ratner

Kulingana na data ya Benki Kuu ya Kenya, dola imekuwa ikiuzwa kwa zaidi ya shilingi 150, ingawa baadhi ya benki za biashara na maduka ya kubadilisha fedha za kigeni yamekuwa yakiiuza kwa kiwango hicho au zaidi katika wiki za hivi karibuni.

Ken Gichinga, mchumi mkuu katika kampuni ya Mentoria Economics, aliliambia shirika la habari la AFP kuwa kiwango cha ubadilishaji fedha kinaonyesha kuimarika kwa dola wakati huu wa mzozo wa Mashariki ya Kati "ambao unawasukuma wawekezaji kwenye rasilimali salama", pamoja na mavuno mengi ya hazina ya Marekani.

Kufikia mwishoni mwa mwezi Juni, Kenya imejilimbikizia deni la zaidi ya shilingi trilioni 10.1 ambazo ni sawa na takriban theluthi mbili ya pato la taifa, kulingana na takwimu za Hazina.

Baadhi ya taarifa hii inatoka shirika la habari la Reuters na AFP

Forum

XS
SM
MD
LG