Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 06:59

Nchi 9 za AU zaridhia watu binafsi, NGOs kupeleka malalamiko yao Mahakama ya AfCHPR


Ramani ya Afrika
Ramani ya Afrika

Tangu kukubaliwa kwa itifaki ya kuanzisha Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu mwaka 1998, nchi tisa tu ikiwemo Tanzania ndio zimekwisha toa tamko la kuridhia watu binafsi na NGOs kupeleka mashauri yao yaliyokidhi vigezo katika Mahakama hiyo.

Taarifa iliyotolewa na Mahakama hiyo Jumanne pia imeeleza kuwa hadi sasa nchi 30 kati ya nchi 55 za Umoja wa Afrika (AU) ndizo zilizoridhia itifaki ya Mahakama hiyo.

Mahakama ya AfCHPR inaendeleza juhudi zake za kujitangaza kwa nchi wanachama wa AU pamoja na wadau mbalimbali ili kutimiza kikamilifu dhima ya Mahakama hiyo.

Hadi mwezi Julai 2019, Mahakama hiyo yenye Majaji 11 kutoka kanda mbalimbali za Afrika imekwisha pokea mashauri 220 kati yake mashauri 62 yamekwisha shughulikiwa.

Dhima muhimu ya Mahakama hiyo yenye makao yake makuu jijini Arusha ni kuimarisha jukumu la kulinda Haki za Binadamu na Watu kwa kuongeza usimamizi imara wa mfumo wa Haki za Binadamu barani Afrika.

Katika kufanikisha juhudi hizo, AfCHPR imekuwa ikifanya ziara katika nchi mbalimbali wanachama wa AU kutoa elimu ya uwepo kwa Mahakama, jukumu lake, dhima yake na pia uendeshaji wa shughuli za Mahakama hiyo.

Hivi sasa ujumbe wa AfCHPR upo visiwa vya Comoro ambapo pia utaitembelea Zimbabwe ili kuitambulisha Mahakama hiyo na kuzihimiza Nchi hizo pamoja na Wananchi wake kuitumia kikamilifu kupeleka mashauri yaliyotimiza vigezo vinavyohitajika shauri kupokelewa katika Mahakama hiyo.

Ukiwa katika Nchi hizo, ujumbe huo ambao unaongozwa na Rais wa Mahakama hiyo, Mheshimiwa Jaji Sylvain Ore’ utakutana na marais wa Comoro na Zimbabwe pamoja na viongozi wengine waandamizi wakiwemo maspika wa mabunge ya nchi husika, mawaziri wa mambo ya nje na wale wa Sheria, mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) na pia vyama vya wanasheria vya nchi hizo.

“Tunazitembelea nchi mbalimbali za AU ili kuzitolea wito na kuzihimiza zitoe tamko kwa mujibu wa kifungu cha 34(6) kuruhusu watu binafsi na NGOs kupeleka kesi moja kwa moja Mahakamani hapo na hivyo kuimarisha mfumo wa Haki za Binadamu barani Afrika alisema Jaji Ore’.”

Tayari Comoro ilikwisha ridhia itifaki ya mkataba wa kuanzishwa kwa AfCHPR tangu mwaka 2013, lakini bado haijatoa tamko la kukubali kuruhusu watu binafsi na NGOs kupeleka kesi moja kwa moja katika Mahakama hiyo ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu.

Kwa upande wake Zimbabwe haijaridhia itifaki ya Mkataba wa kuanzishwa AfCHPR wala kutoa tamko kwa mujibu wa kifungu cha 34(6).

XS
SM
MD
LG